• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Familia zisizo na makazi zageuza maboti kuwa nyumba

Familia zisizo na makazi zageuza maboti kuwa nyumba

NA KALUME KAZUNGU

KWA kawaida binadamu makazi yake, hasa mahali pa kujistiri au kulala ifikapo usiku, huwa ni ndani ya nyumba.

Nyumba inaweza ikawa ya msonge iliyo na paa la nyasi na kuta za matope au ikawa ya kisasa ya matofali iliyoezekwa kwa mabati au kwa makuti.

Pia kuna zile nyumba zinazojengwa kwa kuta za mabati.

Kwa zile familia zisizobahatika maishani aidha, utazipata zinapokosa makazi rasmi hukimbilia kuwa ombaomba vishorobani na pembezoni mwa barabara huku nyingine zikiishi kwenye mapango.

Katika kisiwa cha Lamu, hali ni tofauti. Hapa, utakutana na familia zisizo na makazi rasmi zikigeuza vyombo, hasa vile vikuukuu vya usafiri wa baharini, kuwa makazi rasmi.

Vyombo vinavyotumika ni maboti na mashua.

Miongoni mwa familia hizi ni zile za waathiriwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya almaarufu ‘mateja,’ vijana wa mtaani (chokoraa) na pia zile za wavuvi ambao mara nyingi hujipata baharini wakitekeleza shughuli zao usiku.

Kwa mfano, ni jambo la kawaida kuwaona waathiriwa wa dawa za kulevya wakiwa wametundika matandiko yao kwenye boti au mashua chakavu mchana ambapo huwa wametoka kuenda kujitafutia chakula na mahitaji mengine.

Nguo zikiwa zimeanikwa huku makaa, mitungi na vifaa vingine vya nyumbani vikiwa vimewekwa kwenye boti lililogeuzwa kuwa nyumba kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Jioni utakutana na familia hizo zikijibanza ndani ya mashua hayo, ambapo hulala usiku kucha.

Kuna wengine ambao hata utawapata wakipika ndani ya mashua hizo kuukuu kwani wakaaji hutenga eneo maalum la boti kutumia kama jikoni yaani eneo la kupikia.

Picha ya mojawapo ya jiko linalotumika kupikia ndani ya boti. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Khadija Shebwana na Babli Shee Athman ni bibi na bwana ambao zamani walikuwa waathiriwa wa dawa za kulevya kabla ya kunusurika.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bi Shebwana alieleza jinsi ambavyo maboti makuukuu yalivyowapa hifadhi katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 15 waliyokuwa wakiishi kama waraibu wa dawa za kulevya.

 

Bi Khadija Shebwana (kulia) na mumewe Babli Shee Athman. Wanandoa hao wanasema kipindi ambapo maisha yaliwaendea visivyo, maboti makuukuu yalikuwa kiokozi kwao kwani waliyageuza makazi au nyumba yao ya kulala usiku. PICHA | KALUME KAZUNGU

“Twashukuru kwamba mwishowe tulinusurika kutoka kwa mihadarati lakini kusema kweli isingekuwa haya maboti makuukuu sijui tungeishije sisi wawili. Tuliyatumia sana haya maboti kama nyumba zetu usiku ilhali mchana tunajipanga,” akasema Bi Shebwana.

Bi Khadija Shebwana (kushoto) akiwa na mumewe Babli Shee Athman. Wanandoa hao wanasema kipindi ambapo maisha yaliwaendea visivyo, maboti makuukuu yalikuwa kiokozi kwao kwani waliyageuza makazi au nyumba yao ya kulala usiku. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mohamed Yusuf ambaye ni mvuvi tajika kisiwani Lamu anashukuru wamiliki wa maboti makuukuu kwa kuwaelewa na hata kuwaruhusu kuyatumia kama makazi yao.

Bw Yusuf anataja uvuvi kuwa kazi inayomwacha mja kutumia muda mwingi usiku akiwa baharini kuvua samaki.

Anasema kila wanapoenda baharini kuvua na kisha kumaliza shughuli zao nyakati za usiku, wao hutafuta makao kwenye hayo maboti kuukuu.

“Maboti mengi makuukuu yamepakishwa kwenye fuo za Bahari Hindi hapa Lamu, Mokowe, Wiyoni, Matondoni, Shella, Kizingitini, Faza na kwingineko. Haya ndiyo tunayoyatumia kama nyumba zetu nyakati za usiku. Tunajikinga na mvua na kibaridi kikali. Pia tunapika ndani ya haya maboti kabla ya kwenda zetu alfajiri baada ya kazi,” akasema Bw Yusuf.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa mbali na familia zisizo na makazi rasmi kutumia maboti makuukuu, pia kuna baadhi ya watu ambao wakati wanapolemewa na kodi ya nyumba wamekuwa wakiishia kulala kwenye maboti makuukuu japo kwa muda.

Bw Charo Kathengi, mfanyakazi za vibarua kisiwani Lamu, alifichua kuwa yeye binafsi amewahi kufungiwa nyumba na landilodi wake baada ya kufeli kulipa kodi ya miezi miwili.

“Hapo ilinibidi kutafuta hifadhi kwenye mojawapo ya maboti hayo makuukuu. Sina mke wala watoto kwa hivyo ilikuwa rahisi kwangu kujibanza botini usiku kucha na kisha kudamka alfajiri na mapema kuchapa kazi. Nilirudia nyumba yangu baada ya wiki mbili hivi nilipofaulu kupata kodi iliyohitajika,” akasema Bw Kathengi.

  • Tags

You can share this post!

Joto kuhusu mgombea wa urais wa Azimio lashamiri mazishini

Jinsi maisha ya Mbarire yalivyogeuka baada ya kufichua...

T L