Habari za Kaunti

Fujo Egerton mwanafunzi akishambuliwa

Na JOHN NJOROGE na FRANCIS MUREITHI April 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAHARUKI inaendelea kutanda katika Chuo Kikuu cha Egerton, Kaunti ya Nakuru baada ya mwanafunzi wa kike kudungwa kisu na kuachwa na majeraha mabaya Jumatatu usiku, Aprili 7, 2025.

Mali ya maelfu ya pesa pia iliharibiwa na wanafunzi hao ambao walikerwa na kudungwa kwa mmoja wao kwa kisu na watu wasiojulikana.

Kwa mujibu wa wanafunzi ambao walizungumza na Taifa Dijitali, ghasia zilianza saa mbili usiku baada ya mwanafunzi aliyekuwa akielekea katika chumba chake kudungwa kwa kisu.

Mwanafunzi huyo aliachwa na majeraha mabaya usoni, kifua, kichwani na akakimbizwa hadi hospitali kwa matibabu dharura.

Baada ya kuvamiwa kwa mmoja wao, wanafunzi walikongamana kwenye lango la chuo na kuanza fujo.

Walivunja stoo ya vyakula, wakapora kila kitu ikiwemo vyakula ambavyo vilikuwa kwenye jokofu.

Pia, waliharibu vitabu ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa huku pia wakiiba mali.

Mmoja wa wafanyakazi chuoni humo alisema wanafunzi waliteketeza jokofu, madawati pamoja na vifaa vingine.

Hali kadhalika, gari la chuo ambalo lilikuwa limeegeshwa lilipasuliwa vioo.

Kwa mujibu wa mlinzi wa kibinafsi, polisi wawili ambao walikuwa kwenye lango walilemewa na hawangeweza kuzuia umati huo wa wanafunzi kushiriki uporaji.

“Wanafunzi hao walikuwa wengi sana na polisi hawangefanya chochote kuwazuia,” akasema mlinzi huyo.

Jumanne, Aprili 8, Naibu Chansela Prof Isaac Kibwage alishutumu ghasia hizo akilalamika kuwa wanafunzi na wahuni waliungana kupora na kuharibu mali ya chuo.

Wanafunzi wengine walisema walisukumwa kuharibu mali ya chuo kwa sababu usimamizi ulikuwa umekataa kushughulikia ukosefu wa usalama katika chuo hicho.

“Tumepiga ripoti kuhusu kuvamiwa na wezi ambao wamejihami usiku lakini hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa,” akasema mmoja wa wanafunzi hao.

“Usiku ukiingia tu katika Chuo Kikuu cha Egerton, huwa tuko mikononi mwa genge ambalo limejihami na huwa tupo hatarini,” akasema mwanafunzi mwingine ambaye yupo mwaka wa tatu.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Njoro, David Apima alithibitisha kuwa hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na kuharibiwa kwa mali ya chuo na pia kudungwa kisu kwa mwanafunzi huyo wa kike.

Bw Apima awali alikuwa amesema fujo hizo zilianza baada ya baadhi ya wanafunzi ambao wanaishi nje na hawakufurahishwa na mitihani inayoendelea, walijaribu kuingia chuoni humo kwa lazima.