Gavana aahidi waliohusika na hitilafu ya oksijeni hospitalini watachukuliwa hatua
SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeahidi kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayepatikana na hatia ya kusababisha hitilafu kwenye mfumo wa usambazaji oksijeni katika Hospitali Kuu ya Pwani ambayo inahusishwa na vifo vya wagonjwa watatu Jumatano iliyopita (Machi 26, 2025).
Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Sheriff Nassir, Ijumaa, Aprili 4, 2025 alisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo, na akaahidi kuwa hakuna atakayesazwa.
“Tutafuatilia suala hili kwa kina hadi ukweli upatikane. Ikiwa ni mfanyakazi wa hospitali aliyehusika, basi sheria itachukua mkondo wake. Hatutakubali utepetevu,” alisema Gavana Nassir.
Gavana huyo pia alifichua kuwa amekutana na familia ya mmoja wa marehemu, Mwangi Kimanzi, na kueleza kuwa uchunguzi wa pamoja wa maiti utafanywa na wataalamu wa afya walioteuliwa na familia na serikali ya kaunti ili kubaini kilichosababisha kifo hicho.
“Ni kweli wagonjwa wamefariki dunia, lakini hatuwezi kusema kwa uhakika kuwa ni kutokana na tatizo hilo la oksijeni. Uchunguzi lazima ukamilike kabla ya kutoa hitimisho,” aliongeza.
Tukio hilo la kusikitisha limezua ghadhabu miongoni mwa viongozi wa kisiasa, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, na wananchi ambao wanataka hatua madhubuti zichukuliwe na mageuzi ya haraka yafanywe katika sekta ya afya ya kaunti hiyo.
Tume ya Haki za Binadamu na Haki ya Kijamii imetaka afisa mkuu wa afya katika serikali ya kaunti aondolewe kazini kwa tuhuma za kuzembea kazini na kutowajibika.
“Tunataka uchunguzi wa kina na huru ufanyike mara moja. Wote waliohusika wawajibishwe bila kuchelewa. Afisa wa kaunti anayesimamia afya hana budi ila kuondolewa,” alisema Julius Ogogoh, afisa mwandamizi wa tume hiyo.