Gavana Barasa apata pigo korti ikirejesha wanachama wa bodi aliowatimua
NA SHABAN MAKOKHA
GAVANA wa Kaunti ya Kakamega, Fernandes Barasa, alipata pigo mara mbili baada ya Mahakama ya Kakamega kuwarejesha wanachama wanne wa Bodi ya Huduma ya Umma ya Kaunti (CPSB) waliotimuliwa afisini na Bunge la Kaunti.
Wakati huo huo ombi la uongozi wa kaunti kudumisha hali iliyopo ya kuwazuia wanachama wa CPSB waliorejeshwa kutokanyaga ofisi zao kusubiri rufaa kuhusu uamuzi huo, lilitupiliwa mbali na korti hiyo.
Mnamo Novemba 14, 2023, Bunge la Kaunti lilimtimua Catherine Omweno (mwenyekiti) na wanachama Stanley Were, Joel Omukoko na Ralph Wangatiah kwa misingi ya matumizi mabaya ya afisi, ukiukaji wa Katiba, kuvunja sheria, kukosa nidhamu, na utendakazi duni.
Korti ya Ajira na Mahusiano ya Leba, hata hivyo, ilifuta hatua hiyo ikisema ni kinyume na sheria, ukiukaji wa kanuni na Katiba.
Jaji Jemima Keli alisema wanne hao waling’atuliwa afisini kwa njia isiyo ya haki na kuamuru warejeshwe mara moja.
Wakili wa Gavana Barasa, Bw Patrick Lutta, aliwasilisha ombi kwa lengo la kuzuia kutekelezwa kwa uamuzi uliosema Bunge la Kaunti liliwatimua wanachama wa CPSB kinyume na sheria kisha Gavana akawafuta kazi.
Katika uamuzi wake, Jaji Keli alisema hoja ya Bw Barasa si thabiti.