Gavana Mwadime aagiza baa zifunguliwe
NA LUCY MKANYIKA
GAVANA Andrew Mwadime ametoa agizo kwa wamiliki wa baa katika Kaunti ya Taita Taveta ambao wamefuata masharti ya Sheria ya Kudhibiti Vileo kuendelea na biashara zao hata baada ya kufungwa kwa baadhi yao wakati wa msako unaoendelea na maafisa wa usalama.
Gavana huyo amesisitiza kwamba ni baa pekee ambazo leseni zao zilitolewa kinyume cha sheria ndizo zinapaswa kufungwa.
“Wale ambao walipewa leseni na Bodi ya Udhibiti na Utoaji Leseni ya Vinywaji na Vileo ni kumaanisha kuwa kamati iliona wamefikia vigezo vyote vilivyowekwa. Tutumie sheria na wale wamekamilisha maagizo yote baada ya kukaguliwa na Bodi ya Udhibiti na Utoaji Leseni ya Vinywaji na Vileo vya Kaunti na wakathibitishwa warudi kwa biashara zao,” alisema gavana Mwadime.
Aidha, Bw Mwadime ameeleza kuwa serikali ya kitaifa inaingilia kati kazi ambayo ni ya serikali ya kaunti, akisisitiza kwamba udhibiti wa vileo uko chini ya mamlaka ya serikali ya kaunti.
“Serikali kuu isijaribu kuingilia swala la leseni. Hili ni swala la kaunti. Ikiwa kuna mtu ana tatizo sio kuwasumbua nyinyi bali wanaweza kwenda kortini wawasilishe malalamishi yake huko,” alisema.
Haya yanajiri baada ya wamiliki wa baa katika baadhi ya maeneo ya kaunti hiyo kukashifu kile wanachodai kufungwa kwa biashara zao kwa lazima na kwa muda usiojulikana na maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa.
Akihutubia wanahabari mjini Voi, Bw Mwadime alieleza kuwa baadhi ya baa zilizolengwa zina leseni halali na ni biashara zinazofuata sheria.
Wamiliki wa baa wamelalamika kwamba biashara zao zilifungwa kiholela na maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa, licha ya kuwa na leseni zinazohitajika na biashara zao ziko katika maeneo ya kibiashara na vituo vya biashara, na hivyo haziko katika maeneo yaliyozuiliwa au kukiuka kanuni nyingine.
Baadhi ya wamiliki hao waliandamana hadi katika afisi ya manispaa ya Voi ili kusukuma serikali ya kaunti kusaidia.
Gavana Mwadime hata hivyo ameunga mkono vita dhidi ya vikundi haramu na wale wanaouza pombe kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
‘Tumekuwa wamekuwa wengi katika eneo hili. Nakashifu wale ambao wanauza pombe haramu. Tuko na watu wengi ambao wameathirika kwa sababu ya pombe haramu,” akasema.
Naibu Rais Rigathi Gachagua amechukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuamrisha kusimamisha kwa muda leseni na vibali vya kuthibitisha vinywaji vya pombe na wazalishaji wa vinywaji vya pombe vilivyotolewa na Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) na Shirika la Viwango vya Kenya (Kebs).
Leseni zote halali zilizopo zitahakikiwa upya ndani ya siku 21 za agizo hilo, na biashara zitaruhusiwa kuendelea tu baada ya kupokea idhini mpya. Hii ni hatua ya serikali katika kuhakikisha udhibiti bora wa uzalishaji na uuzaji wa pombe nchini.