Habari za Kaunti

Gavana Mwadime alia Samboja kamuachia zigo la deni kubwa la Sh1.4bn

January 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LUCY MKANYIKA

GAVANA wa Kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime amewataka waliompigia debe kuwa na subira anapojitahidi kuboresha uchumi wa kaunti hiyo.

Akiongea katika hafla ya kutoa ufadhili kwa watoto 100 wanaojiunga na Kidato cha Kwanza kutoka familia zisizojiweza, gavana huyo alisema kuwa amekumbana na changamoto nyingi katika serikali aliyorithi kutoka kwa mtangulizi wake Granton Samboja.

Alisema alikuta deni la Sh1.4 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na wakandarasi ambalo hadi leo hii angali analipa.

“Nilipochukua hatamu za uongozi, nilikuta deni kubwa sana. Deni la wakandarasi lilikuwa Sh1.4 bilioni na bado linaendelea kulipwa. Serikali yangu inapitia changamoto za kifedha,” alisema gavana Mwadime.

Alisema kuwa amepokea lawama kuwa alikuwa amewaacha waliomshika mkono wakati alipokuwa akipiga kampeni za ugavana katika uchaguzi uliopita.

“Ninasikia tetesi kuwa ‘Mwadime amewacha makampena wake, mara haangalii makampena wake kama aliyekuwa mtangulizi wake’. Mnataka na mimi niibe? Mimi siwezi kuiba. Mimi niko hapa kufanya kazi kwa wakazi na wenyeji wote wa Taita Taveta,” akasema.

Alisema kuwa tayari serikali yake imelipa madeni yakiwemo deni la madawa katika shirika la Kemsa, deni la NSSF na NHIF na vilevile mikopo ya wafanyakazi.

“Tulipoingia wafanyakazi walikuwa wakikatwa mishahara kulipia ada tofauti lakini fedha hizo zilikuwa hazifiki kwa vitengo hivyo. Wafanyakazi tulipata wakidai mishahara ya miezi minne na hizo zote tumelipa,” alisema.

Alisema kuwa serikali yake inajitahidi kuboresha huduma za afya, madini, elimu, kilimo, miundombinu na maendeleo ya jamii.

Hata hivyo, alisema kuwa fedha wanazopata kutoka kwa serikali kuu ni chache mno na haziwezi kutekeleza maendeleo katika kaunti hiyo.

Bw Mwadime alisema kuwa kati ya Sh400 milioni wanazopata kila mwezi, Sh320 milioni hulipa mishahara ya wafanyakazi, Sh20 milioni hununua madawa huku zilizosalia zikitumiwa kwa matumizi mbalimbali ya serikali.

“Ni milioni chache tu zinazobaki za kufanya maendeleo. Ndiposa mnaona niko mbioni kutafuta wafadhili ili tuungane tufanye miradi kwa sababu bila hivyo hatutafanya kitu,” alisema.

Mpango huo wa kutoa ufadhili kwa watoto wanaojiunga na Kidato cha Kwanza kutoka familia zisizojiweza ulianza mnamo 2014 na hadi sasa jumla ya watoto 670 wamefaidika.

Mwaka 2024 watoto 400 wa Kidato cha Kwanza hadi cha Nne wako kwa mpango huo. Serikali imetenga Sh12 milioni kuendea ufadhili huo.

Mwaka 2023 bunge la kaunti hiyo lilibuni sheria ya kuongeza mgao wa elimu kutoka Sh100 milioni hadi Sh200 milioni huku kila wadi ikitengewa Sh20 milioni.

Bw Mwadime aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu bora na kuwapa motisha ya kufaulu.

Alisema kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na kuwa serikali yake itaendelea kusaidia wanafunzi ambao hawana uwezo wa kugharamia masomo yao na kutaka vilevile wafadhili wengine kuungana katika jitihada hizo.

Wakati huo huo, serikali hiyo imeajiri walimu 309 wa shule za chekechea na wengine 60 wa vyuo vya ufundi chini wa mpango wa kudumu.

“Serikali yangu itahakikisha kuwa wafanyakazi wote wana mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwemo kuwalipa mishahara yao kwa wakati unaofaa. Hivyo ni jukumu lao pia kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa wananchi,” akasema.

Alitoa wito kwa wenyeji na wakazi wa Taita Taveta kuunga serikali yake mkono katika kutekeleza ajenda yake ya maendeleo na kuwa na imani kuwa atabadilisha hali ya kaunti hiyo.

“Naomba mniunge mkono katika kazi hii ngumu. Nina nia ya kuwaletea maendeleo na ustawi. Msikubali kuingizwa kwa siasa za mapema kwa kuwa wanaofanya hivyo hawawatakii mema,” alisema.