Habari za Kaunti

Gavana atetea wabunge waliopitisha mswada wa fedha

Na SIAGO CECE July 7th, 2024 2 min read

GAVANA wa Kwale Fatuma Achani amewatetea wabunge wa kaunti hiyo waliounga Mswada wa Fedha 2024 akisema kuwa hatua hiyo ilikuwa na nia ya kuleta maendeleo.

Gavana huyo alisema kuwa kungekuwa na miradi mingi ambayo ingetekelezwa endapo mswada huo ungefaulu na kutiwa saini na Rais William Ruto.

Akizungumza katika eneo la Ukunda eneobunge la Msambweni, Bi Achani alisema aliwashawishi wabunge wa Kwale, kuunga mkono mswada huo kufuatia miradi mingi za serikali ya kitaifa kusimama katika kaunti hiyo.

“Niliambia wabuge wangu wapitishe mswada huo maana sisi pia twataka pesa. Miradi yetu ambayo imekwama kama daraja la Funzi na Mwachande na barabara ya Kinango zote zingekamilika ikiwa mswada huo ungepitishwa,” akasema Bi Achani

Aidha gavana huyo alieleza kuwa kupitia mswada huo, Kaunti ya Kwale ingepokea Sh1.2 bilioni, ambazo zingekuwa pesa nyingi za maendeleo. Baadhi ya pesa hizo, alieleza kuwa zingeendea serikali ya kaunti na afisi za wabunge.

“Kwa sasa kuna miradi ambayo lazima itakatizwa. Kwale sio kama kaunti zingine nchini kama Kiambu au Mombasa, mahitaji yetu ni muhimu na tofauti,” akaongeza.

Kwa upande wake, Mwakalishi wa Wadi ya Kinondo Juma Maone aliwataka wakazi wa Kwale kuwapa wakati viongozi kufanya kazi kwa ushirikiano, akieleza kuwa hatua yao ya kukubali Mswada wa Fedha ilikuwa na nia ya kuleta maendeleo.

“Kama kazi huku inafanyika vizuri, shida iko wapi ya kuwafanya wao wapinge mswada?” Bw Mwaone aliuliza.

Hata hivyo, viongozi wa kutoka mrengo wa Azimio walimkosoa Bi Achani na wabunge waliounga mkono Mswada wa Fedha na kusema kuwa walifanya hivyo kwa sababu za kibinafsi.

Aliyekuwa mgombea wa kiti cha ubunge cha Msambweni Omar Boga, alisema kuwa wakazi wanastahili kuhakikisha kuwa kila kiongozi aliyeunga mkono mswada huo hapigiwi kura mnamo 2027.

“Hao viongozi wote lazima waende nyumbani kwa sababu hawajaweka maslahi yetu mbele. Tusije tukadanganywa ilhali bado kuna changamoto nyingi na maendeleo ambayo haijafanyika kusaidia wakazi wetu,” akasema Bw Boga.

Haya yanajiri huku maandamano yakiingiliwa na vijana wahalifu katika kaunti hiyo ambao walinyanyasa wafanyabiashara na kuwaibia wakazi.

Bi Achani aliwataka vijana kusitisha maandamano akisema hali hiyo inaathiri sekta ya utalii ambayo ni chanzo kubwa cha ajira katika kaunti hiyo.

Pia, alilaumu mashirika ya kijamii kwa kupanga maandamano akiwaonya wananchi kutotumika.