Habari za Kaunti

Helikopta kutumiwa kwa uokoaji wa dharura Ziwa Victoria

Na RUSHDIE OUDIA, GEORGE ODIWUOR September 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amezindua ujenzi wa kituo cha kushirikisha utafutaji na uokoaji katika Ziwa Victoria ambacho kitakuwa na vifaa bora ikiwemo helikopta.

Kituo hicho kitakachojengwa katika Kaunti ya Kisumu kitasaidia wakazi wa kaunti za karibu na ziwa hilo ambao amekuwa wakilalamikia huduma duni za kushughulikia dharura zikiwemo ajali ziwani.

Rais alisema mbali na kituo hicho kikuu kitakachogharimu Sh800 milioni, vituo vingine vidogo vitaanzishwa katika kaunti za Migori, Homa Bay, Siaya na Busia kwa gharama ya Sh3.2 bilioni chini ya mradi mkubwa wa uchukuzi wa mataifa mbalimbali.

Rais Ruto alisema mradi huo inanuiwa kuimarisha usalama ndani ya Ziwa kupitia mawasiliano bora na mfumo thabiti utakaosaidia kupokea habari kuhusu dharura na kuzishughulikia akisema Kenya hupoteza wavuvi wengi ndani ya Ziwa Victoria kila mwaka kwa sababu ya vifaa duni.

“Kituo hiki kitakuwa na vifaa bora na pia kuwa na helikopta ambayo itakuwa ikitumiwa kuokoa wale wanaohusika katika ajali ndani ya ziwa hili. Tukifanya uvuvi kuwa salama, tutatia moyo watu wengi kushiriki katika biashara hiyo,” alisema Rais Ruto.