Hofu Kwale watoto wengi wakipata maambukizi ya macho mekundu
NA SIAGO CECE
ZAIDI ya watu 300 wamepata maambukizi ya ugonjwa wa macho mekundu huku visa vya maambukizi hayo vikiongezeka katika Kaunti ya Kwale.
Kulingana na afisa wa uchunguzi wa magonjwa katika kaunti hiyo Mohammed Mwachinangu, zaidi ya asilimia 70 ya visa hivyo ni vya watoto wa shule.
“Watoto wa shule ndio walioathiriwa zaidi na virusi vinavyoenea kwa sababu ya idadi yao na vile wanavyokaa. Ili kuzuia maambukizi, tunasambaza vifaa vya kusafisha mikono na kunawia mikono kwa shule zilizoathirika,” Bw Mwachinangu alieleza Taifa Leo katika mahojiano.
Takwimu zilionyesha kuwa kati ya visa 283, maambukizi 240 yalikuwa kwa wanafunzi, huku maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa Kinango, Moyeni, Mazeras, Diani, na Maganyakulo.
Bw Mwananchinangu alisema pia maambukizi mengine ni ya kutoka kaunti ya Mombasa na nchi jirani ya Tanzania.
“Watu wengi walio na jamaa au wanafamilia wanaosafiri kati ya Mombasa na Kwale pia wameathirika na wako katika hatari kubwa,” afisa hiyo alisema, akiongeza kuwa baadhi ya vituo bado havijaarifu idara ya afya kuhusu visa hivyo vilivyorekodiwa.
Haya yanajiri huku wakazi wengi walioathirika wakipendelea kunawa nyuso zao kwa maji ya chumvi kutoka ufukweni ili kuharakisha kupona.
Bi Monicah Mwende, ambaye ni mkazi wa Diani, alifichulia Taifa Leo kwamba alienda kuosha macho yake kwenye fuo za bahari ili kuharakisha kupona kwake na watoto wake.
“Nilienda hospitalini lakini pia nilihakikisha kuwa nilikuwa nimepitia ufuo wa bahari ili kujiosha baada ya majirani kunishawishi kuwa ni njia mojawapo ya matibabu,” Bi Mwende akasema.
Lakini wataalamu wa matibabu wanasema hakuna uhusiano wa kisayansi kati ya maji kutoka baharini na kupona kwa maambukizi ya macho mekundu miongoni mwa watu.
“Siku zote tunaenda na dawa zenye ushahidi kama madaktari na hakuna uthibitisho kwamba maji ya chumvi au hata chai inaweza kusaidia kuponya ugonjwa,” Dkt Nadya Mustafa ambaye ni daktari wa macho alisema.
Visa vya ugonjwa huo pia vimeripotiwa Mombasa, Nairobi, Kisii, Lamu, na Malindi katika Kaunti ya Kilifi.