Hofu simba wenye njaa wakizurura ovyo vijijini
NA STANLEY NGOTHO
TAHARUKI imezuka katika vijiji kadhaa kaunti ndogo ya Kajiado Mashariki baada ya simba tisa kuonekana wakizurura ovyo kwa muda wa siku tatu sasa.
Simba hao wanasemekana kutoroka mbuga ya Nairobi kutafuta chakula.
Vijiji hivyo vinapakana na mbuga hiyo upande wa Kusini.
Wanyama hao wamekuwa wakizurura katika vijiji vya Sholinke, Nkuruka, na Empakasi na kutwaia hofu wenyeji na wakazi.
Mnamo Jumatano asubuhi, wanyama hao walionekana karibu na timbo la mawe la Sholinke na kusababisha hofu.
“Wanazurura vijijini. Tunarejea katika nyumba zetu kabla ya giza tukihofia kushambuliwa,” alisema Bw James Kioko, mfanyakazi katika timbo hilo.
Maafisa kutoka Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) wametumwa katika eneo hilo kuwarudisha wanyama hao katika mbuga hiyo.