• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Hoja yalenga kumng’atua waziri wa Ardhi Taita Taveta

Hoja yalenga kumng’atua waziri wa Ardhi Taita Taveta

NA LUCY MKANYIKA

UTAWALA wa Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime umeanza kukabiliwa na mawimbi makali baada ya hoja ya kumng’atua mmojawapo wa mawaziri wake kuwasilishwa katika bunge la kaunti hiyo. 

Waziri wa Ardhi na Madini Elizabeth Mkongo atakuwa wa kwanza kukabiliana na mawimbi hayo endapo hoja iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi wa Bunge la Kaunti ya Taita Taveta Hope Anisa itapitishwa.

Bi Anisa ambaye ndiye aliyedhamini hoja hiyo, alimshutumu Bi Mkongo kwa uongozi duni na kukiuka maadili.

Anamtuhumu waziri huyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Anamlaumu kwa kutokamilisha uandaaji wa Orodha ya Thamani ya Ardhi ya Kaunti, ambayo imezuia serikali ya kaunti kupata mapato kutokana na mali zilizoko.

Aidha, anasema kuwa Bi Mkongo amepuuza kuwasilisha sera, sheria na kanuni zinazohitajika kwa bunge la kaunti hiyo ili kusimamia na kulinda ardhi na madini ya kaunti, jambo ambalo limesababisha matatizo kama kunyakuliwa kwa vipande vya ardhi, kufurushwa kwa familia na ujenzi wa kiholela katika maeneo ya mijini.

Matatizo haya, alisema, yameathiri pakubwa usimamizi na maendeleo ya ardhi ya kaunti, pamoja na ustawi wa wakazi wake.

“Sekta ya madini imeendelea kupuuzwa ilhali inaweza kuzalisha kipato kwa wakazi. Hii imewanyima wakazi haki zao za kiuchumi na mapato kwa serikali ya kaunti,” akasema.

Pia anadai kuwa amekuwa hajitokezi ili kujibu maswali na maswala muhimu bungeni.

“Kushindwa kwa idara hii kutadidimiza uchumi wa kaunti hii na maisha ya wenyeji na vilevile kusababisha hali ya umaskini miongoni mwa wakazi,” akasema.

“Kuendelea kwa Bi Mkongo kuwa waziri wa idara hii kuna uwezekano wa kuitumbukiza kaunti katika ukosefu wa makao, mipango mibovu ya miji, ujenzi usiodhibitiwa na uchimbaji wa kiholela na uvamizi na unyakuzi wa ardhi ya umma,” akaongeza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi wa Bunge la Kaunti ya Taita Taveta Hope Anisa. PICHA | LUCY MKANYIKA

Aidha, anadai kuwa waziri huyo anamdhalilisha Afisa Mkuu wake, Jimmy Mtawa, na kuchagua kufanya kazi na Naibu Mkurugenzi wa Madini Peter Sholo.

Hoja ya kumng’atua waziri huyo imejiri baada ya wawakilishi wa bunge hilo kurejelea vikao vyao na kuonya serikali ya kaunti kuwa watachukua hatua kali kwa wafanyakazi ambao hawatimizi majukumu yao.

Wakizungumza wakati wa ibada ya maombi katika bunge mnamo Jumanne, Spika wa Bunge Wisdom Mwamburi na naibu wake Anselm Chao walisema hawatavumilia uzembe miongoni mwa maafisa wa serikali ya kaunti hiyo.

Walikanusha madai kuwa bunge hilo limeingizwa mfukoni na maafisa wa kaunti na kusema kuwa linafanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya kaunti kwa manufaa ya wenyeji.

“Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha huduma ziko sawa. Uongozi si tu kuhusu kufanya maamuzi makali bali kushughulikia maswala ya wenyeji na kwa manufaa yao,” spika Mwamburi alisema.

Kwa upande wake, Bw Chao alikariri kuwa bunge hilo halitaogopa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ili kuboresha maisha ya wakazi.

“Tuko hapa kuhudumia wenyeji wa Taita Taveta. Tutatekeleza majukumu yetu na tuko tayari kufanya maamuzi magumu. Watu wanatuambia mambo si shwari. Lazima tutimize matarajio ya watu wetu. Iwapo serikali ya kaunti haitoi huduma, tutachukua hatua ili kuwapa nafasi wengine ambao wako tayari kufanya kazi,” alisema Bw Chao.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Bi Mkongo alipuuzilia mbali tishio la kumng’atua, akisema amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa bidii na kitaalamu.

Alisema amekuwa akifanya kazi kwa karibu na gavana na wadau wengine ili kutatua changamoto za ardhi katika kaunti hiyo.

“Najua hawa ni magenge ya wahalifu ya maswala ya ardhi wanaopambana nami. Ninajua nitapita hili,” Bi Mkongo akasema.

Mapema wiki hii, gavana Mwadime aliwaomba wakazi kuwa na subira na mawaziri wake kwani wako katika mchakato wa kutekeleza ajenda yake.

Gavana alisema mawaziri wake walitia saini mkataba wa utendakaji ambao utapima kila mmoja kwa mafanikio yake.

“Tuwape muda. Ikiwa watakuwa hawajatekeleza yale tuliyokubaliana ndipo tuwang’atue,” Bw Mwadime aliwatetea.

  • Tags

You can share this post!

Raila kujiondoa kwa siasa za Kenya akichaguliwa mwenyekiti...

Mwanamke azuiliwa kwa kupiga hadi kuua bintiye wa miaka 7

T L