• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Hospitali tegemeo Taita Taveta zaugua kwa kukosa vitengo vya ICU, mitambo ya oksijeni

Hospitali tegemeo Taita Taveta zaugua kwa kukosa vitengo vya ICU, mitambo ya oksijeni

NA MARY WANGARI

WENYEJI na wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta huenda wakalazimika kusubiri kwa muda zaidi kabla ya kupata huduma za afya kikamilifu.

Hii ni baada ya kubainika hospitali zote za umma zinazotegemewa eneo hilo, hazina Kitengo cha Wagonjwa Mahututi wala kituo cha kuhifadhia mitungi ya hewa muhimu ya oksijeni.

Kituo kinachotumika kwa sasa katika eneo la Mwatate hakijaafikia viwango vya ICU kutokana na matibabu na huduma inayotolewa pale.

Haya yote yalianikwa mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Afya katika kikao cha Jumanne.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago, ilielezwa kwamba kituo kinachotumiwa na wagonjwa mahututi Taita Taveta ni HDU na wala si ICU.

Japo ICU na HDU vyote ni vitengo maalum katika vituo vya afya, huduma inayotolewa ICU ni ya kiwango cha juu zaidi kwa wagonjwa mahututi ikilinganishwa na HDU.

Aidha, viwango vya huduma na gharama katika HDU huwa katikati ya ICU na wadi za kawaida.

Ripoti iliyowasilishwa kwa Seneti na Kaimu Karani na Mkuu wa Huduma za Umma Kaunti ya Taita Taveta Habib Mruttu inafafanua kuwa kituo cha Mwatate “chenye vitanda vinne kilijengwa ili kutoa Huduma Mahususi wakati wa janga la Covid-19, na kutoa matibabu ya hewa ya oksijeni kwa wagonjwa waliokuwa wanaugua Covid-19.”

Kamati ilielezwa kwamba Kituo cha Mwatate hakijatimiza viwango vya kuwa ICU kwa sababu hakina vitengo muhimu vinavyojumuisha mashine za maabara mahususi kwa wagonjwa wa ICU, huduma maalum za ICU ikiwemo upasuaji wa mifupa na misuli, upasuaji wa viungo vya uzazi, vipimo vya eksirei za matibabu ikiwemo CT Scan na MRI na huduma za mochari.

Ili kuinua kituo hicho cha Mwatate kufikia viwango vya ICU, Kaunti ya Taita Taveta inayoongozwa na Gavana Andrew Mwadime itahitaji rasilimali tele, Seneti ilielezwa.

Matumaini ya kuwa na ICU katika Hospitali ya Rufaa ya Moi (MCRH) iliyoteuliwa, yatasalia ndoto kutokana na ukosefu wa madaktari bingwa, kukosekana kwa vipimo vya CT Scan na huduma za maabara zilizoidhinishwa rasmi.

Isitoshe, usimamizi wa Taita Taveta umefichua haujui chochote kuhusu ununuzi wa vifaa muhimu vya matibabu, licha ya Kitengo cha eksirei za matibabu kutoa huduma kadhaa kama vipimo vya CT, eksirei ya kawaida, ujauzito na saratani ya matiti.

“Mashine za kufanyia vipimo vya CT na vifaa vinginevyo vinavyotumika MCRH, vilinunuliwa na Serikali Kuu kupitia Mpango wa Huduma Zilizodhibitiwa za Vifaa (MES). Hivyo basi serikali ya kaunti haina habari kuhusu jinsi mchakato wa ununuzi ulivyotekelezwa,” seneti ikaelezwa.

Ingawa mashine hizo zinafanya kazi, zinahitaji kufanyiwa ukarabati lakini mikataba ya kufanya hivyo chini ya MES imepitisha muda wake huku Wizara ya Afya ikilaumiwa kwa kukaa kimya kuhusu suala hilo.

Kwa sasa, kitengo cha eksirei za matibabu katika MCRH, Wesu na Taveta kina jumla ya wataalamu 12.

Wafanyakazi katika idara hiyo hufanya kazi kwa zamu ili kuwezesha kuwepo kwa huduma hizo usiku na mchana.

  • Tags

You can share this post!

NG-CDF yamulikwa kwa wasimamizi kuwa na vyeti ghushi

Hatima ya Dkt Monda kuamuliwa na kamati maalum ya Seneti

T L