Upepo kutokana na kimbunga IALY wasababisha uharibifu Kilifi
NA MAUREEN ONGALA
UPEPO mkali kutokana na kimbunga IALY umeharibu nyumba na mali katika Kaunti ya Kilifi.
Eneo la maegesho ya magari katika Ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa.
Upepo huo ulioshuhudiwa Jumanne mwendo wa saa saba mchana ulisababisha miti kuvunjika na kung’oka karibu na Ofisi za Mipangilio ya Miji katika Kaunti ya Kilifi kabla ya kufikia ofisi ya kamishna ambapo uling’oa paa na kuharibu gari moja lilokuwa limeegeshwa hapo.
Gari lililoharibiwa ni la nambari za usajili GKB 735H.
Soma Pia: Wakenya watahadharishwa kuhusu kimbunga IALY
Sehemu ya paa hilo ilipeperushwa na kufikia nyaya za umeme.
Mbali na magari kuegeshwa, maafisa wa usalama ambao hulinda afisi ya Kamishna wa Kilifi Bw Josephat Biwott, wana mazoea ya kumpuzika katika kivuli cha hapo huku wakipunga upepo.
Wanachama wa kamati ya usalama eneobunge la Kilifi Kaskazini wakiongozwa na Naibu Kamishna wa Kilifi Kaskazini Bw Samuel Mutisya na Kamanda wa polisi wa eneo hilo Bw Kenneth Maina, walifika sehemu hiyo mara moja wakisubiri maafisa wa Kenya Power kukata umeme mara moja.
Bw Mutisya aliwataka wakazi wa Kilifi na Wakenya kwa ujumla kuwa waangalifu.
“Ninawahimiza wananchi kuwa waangalifu. Wasipuuze kwa sababu ni kweli kwamba upepo unavuma. Wasijikinge kwa vivuli vya miti kiholela kwa sababu upepo unaweza kung’oa miti,” akasema Bw Mutisya.