DONDOO: Jamaa ahepa na pesa za matanga alizopewa na mwanasiasa Bomet
POLO aliyepokezwa hela za mazishi na mwanasiasa hapa Chepalungu, Kaunti ya Bomet, alihepa nazo akisema zilikuwa zake.
Duru zinaarifu kuwa polo ni mfuasi sugu wa kigogo huyo wa siasa.
Juzi familia yake ilipopata msiba alimwalika mwanasiasa huyo katika hafla ya mchango wa kumsindikiza mwendazake.
Siku yenyewe kigogo huyo wa siasa alimpa jamaa bahasha nzito baada ya kuhutubia kusanyiko.
Badala ya kuwasilisha hundi hiyo kwa kamati ya mazishi polo aliitia mfukoni mara moja na kukaa kimya.
Kamati ya mazishi ilipomrai aweke pesa hizo mezani ili zisaidie kugharimia mahitaji ya mazishi, kalameni alishikilia kwamba zilikuwa zake eti kwa sababu mwanasiasa huyo alikuja kupitia mwaliko wake.
“Unataka kufaidi kutokana na kifo cha jamaa yako! Wewe namna gani. Ni laana kubwa kufanya hivyo!” polo alisutwa na wanakamati lakini alikaa ngumu wala hakubadilisha msimamo.