• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Jeti ‘Mama Lao’ Lamu hatarini kuporomoka

Jeti ‘Mama Lao’ Lamu hatarini kuporomoka

NA KALUME KAZUNGU

TAKRIBAN Sh400 milioni zinahitajika ili kuikarabati jeti ‘Mama Lao’ inayofahamika kama Fisheries na ambayo ni ya zamani zaidi kisiwani Lamu.

Jeti hiyo imedumu eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50 baada ya kujengwa na idara ya uvuvi mnamo mwaka 1972.

Kwa sasa, jeti hiyo iko katika hali mbaya na wataalamu wameonya kwamba kiegesho hicho kidogo kiko katika hatari ya kuanguka, hali inayotishia shughuli za usafiri wa baharini.

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Ijumaa, Afisa Mkuu Msimamizi wa Idara ya Uvuvi Lamu Kamalu Sharif aliiomba serikali kuu kuingilia kati na kuijenga jeti hiyo ili kusaidia kupiga jeki shughuli za uvuvi eneo hilo.

Bw Sharif alisema serikali ya kaunti haina uwezo wa kuijenga jeti hiyo muhimu kutokana na kwamba bajeti inayohitajika ni ya juu na wasiyoweza kuikimu.

Jeti ya Fisheries almaarufu ‘Mama Lao’ ndio kongwe zaidi kisiwani Lamu. Takriban Sh400 milioni zinahitajika ili kuikarabati baada ya nyufa kutokea kuashiria inaporomoka. Jeti hiyo ambayo iko kwenye hatari ya kuanguka imedumu eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50. PICHA | KALUME KAZUNGU

Afisa huyo wa idara ya uvuvi aidha aliwashauri wavuvi ambao bado wanaitumia jeti hiyo kukoma, akitaja hatua hiyo kuwa ya kuhatarisha maisha yao wawapo katika Bahari Hindi.

“Jeti ya Fisheries ndio ya zamani zaidi hapa kisiwani Lamu. Ilikuwa ikitumiwa na wavuvi na maafisa wa idara ya uvuvi. Inapatikana mbele ya ofisi za idara ya uvuvi. Jeti yenyewe kwa sasa imeoza na karibu ianguke. Wanaoendelea kuitumia waache. Ombi letu kwa serikali kuu ni kuwa isaidie kuikarabati hiyo jeti. Inahitaji kati ya Sh300 milioni na Sh400 milioni,” akasema Bw Sharif.

Simon Komu, ambaye ni Afisa Mstaafu wa Idara ya Uvuvi Kaunti ya Lamu, alitaja utelekezaji na ukosefu wa uangalizi wa jeti hiyo kuwa sababu kuu iliyosababisha kuharibika kwake.

Kulingana na Bw Komu, miaka kabla ya ugatuzi kuanza kutekelezwa nchini, fedha za kuendelezea jeti hiyo zilikuwa zikitolewa moja kwa moja kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.

“Tangu serikali za kaunti kuingia madarakani, uendelezaji wa jeti ya Fisheries umesahaulika kabisa, hivyo kusababisha jeti kuharibika. Najua Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) ndiyo iliyotwikwa jukumu la kuangalia hizi jeti zetu. Twaiomba ishughulikie ujenzi wa jeti ya Fisheries,” akarai Bw Komu.

Naye Mwenyekiti wa Miungano ya Wavuvi katika Kaunti ya Lamu Mohamed Somo anaamini endapo jeti hiyo itajengwa upya na kupanuliwa, itasaidia kuipanua sekta ya uvuvi kote Lamu.

Jeti ya Fisheries almaarufu ‘Mama Lao’ ndio kongwe zaidi kisiwani Lamu. Takriban Sh400 milioni zinahitajika ili kuikarabati baada ya slabu za zamani kuanza kuporomoka. Jeti hiyo ambayo iko kwenye hatari ya kuanguka imedumu eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kwa upande wake aidha, Afisa Msimamizi wa KPA wa Masuala ya Utekelezaji Bandarini Lamu Abdishukri Osman, alisema ofisi yake bado haijapokea ombi maalum kutoka kwa kaunti au wavuvi wa Lamu la kutaka ukarabati, ujenzi na upanuzi wa jeti ya Fisheries ufanywe.

Anasema punde watakapopokea ombi hilo, basi watazingatia kulitekeleza kama njia mojawapo ya KPA kudhihirisha uhusiano wake mwema wa huduma za jamii (CSR).

“Hatujapokea ombi rasmi kutoka kwa kaunti na wavuvi kwamba kuna uhitaji wa jeti ya Fisheries kukarabatiwa, kujengwa na kupanuliwa. Tukipokea ombi hilo tuko tayari kujituma kuona kwamba jeti hiyo inajengwa,” akasema Bw Osman.

Jeti ya Fisheries almaarufu ‘Mama Lao’ ndio kongwe zaidi kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Acheni siasa za pesa nane – Lonyangapuo

Bungei akataa kuzungumzia tukio la mshukiwa wa mauaji...

T L