Habari za Kaunti

Jicho kwa Waziri Joho mzozo wa madini ya chuma Taita Taveta ukichacha

Na LUCY MKANYIKA May 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MZOZO wa uongozi unaoendelea katika shamba kubwa la Kishushe, Kaunti ya Taita Taveta, unazidi kutokota baada ya kamati nyingine ya tatu kuibuka kudai usimamizi.

Mvutano kati ya viongozi, wanahisa na wawekezaji na serikali umezua hofu kuhusu uchimbaji wa madini ya chuma katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa ranchi hiyo, Bw Chombo Shete, ameapa kutimua mwekezaji mmoja anayedaiwa kuchochea migogoro ya uongozi, akidai kuwa anavuruga utulivu na shughuli zao kwa manufaa yake binafsi.

Bw Shete alidai kuwa, mwekezaji huyo hajaanzisha shughuli yoyote tangu alipopata ruhusa ya kuchimba madini ya chuma mwaka wa 2023.

“Anapanga mbinu za kuhadaa wanahisa na kutuondoa ofisini, lakini hatakamilisha njama zake,” alisema Bw Shete.

Shamba hilo lenye wanahisa zaidi ya 700, lina utajiri mkubwa wa madini ya chuma ingawa wenyeji wamekuwa hawaufaidi kutokana na mizozo ya mara kwa mara.

Kwa sasa, shughuli za uchimbaji zimesimama baada ya kampuni ya Samruddha Resources Kenya Ltd na ile ya Universal Exploration Limited kusimamisha uchimbaji.

Kampuni ya Archers Post Investment Ltd ingali kuanza uchimbaji tangu kupewa kibali mnamo 2023.

Kwa muda wa miaka miwili sasa, ranchi hiyo imekuwa na mgogoro wa uongozi kati ya makundi mawili, moja likiongozwa na aliyekuwa katibu wa bodi ya uongozi Bw Danson Kidai, na lingine chini ya Bw Shete.

Mzozo huo kwa sasa unazidi kuwa tata baada ya kundi la tatu kujitokeza hivi karibuni.

Bw Shete amesisitiza kuwa kamati yake ndiyo halali, akiyapuuza makundi mengine kuwa yasiyo na msingi wa kisheria.

“Hatuwezi kuruhusu kamati isiyo halali kuendesha masuala ya ranchi hii. Sisi ndio uongozi halali,” alisema Bw Shete.

Kwa upande wake, Bw Kidai na kundi lake walisisitiza kuwa wao ndio uongozi halali wa ranchi hiyo, wakidai kuwa kamati iliyokuwa madarakani awali haikufuata masharti ya kisheria, hali iliyosababisha uchaguzi wa uongozi mpya mnamo 2023.

“Mkutano huo ulikuwa haramu. Hata afisa wa ushirika hakuhudhuria. Walifanyaje uchaguzi?” alisema Bw Kidai huku akipinga vikali kamati mpya iliyoanzishwa hivi karibuni.

Licha ya mvutano unaoendelea, jitihada za Wizara ya Madini kusuluhisha mgogoro huo zimegonga mwamba, huku pande zote zikikataa kulegeza misimamo yao.