• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:03 AM
Jinsi vishoroba vya mji wa Lamu vinavyomtambua mgeni na mwenyeji

Jinsi vishoroba vya mji wa Lamu vinavyomtambua mgeni na mwenyeji

NA KALUME KAZUNGU

MJI wa Kale wa Lamu ni wa aina yake kutokana na kukithiri kwa vishoroba na vichochoro vingi kwenye mji huo wa kihistoria.

Kwa anayeishi Lamu, utakadiriwa kuwa mwenyeji halisi au mzaliwa wa eneo hilo endapo utakuwa na uwezo wa kutambua vichochoro hivyo na pia kuvitumia katika shughuli za kila siku bila kutapatapa.

Yaani, ni kwenye mji wa kale wa Lamu ambapo vibaraste au vibarabara vya mji huo wa kihistoria humtambua mja kuwa mgeni au mwenyeji.

Aghalabu mja atatambuliwa kiurahisi kuwa mgeni au asiyekuwa mzawa kindakindaki wa Lamu iwapo atajipata kukosa ufahamu na uwezo wa kuvitumia vinjia vilivyoko.

Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliuorodhesha mji wa kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa zaidi ulimwenguni kwa kuhifadhi ukale wake-yaani Unesco World Heritage site.

Miongoni mwa vigezo vilivyotumika na Unesco kuuteua mji wa kale wa Lamu ni jinsi wenyeji walivyofaulu kuenzi tamaduni zao, ikiwemo kutembea kwa miguu, punda na mikokoteni, ikizingatiwa kuwa vibarabara vilivyoko mjini ni vyembamba na vinavyokosa uwezo wa kupitisha magari, baiskeli au pikipiki.

Taifa Leo ilizama nchini kuchanganua vichochoro na mitaa ya Lamu ambayo wakazi, hasa wale ambao si wenyeji hawajaifahamu vyema, hivyo kuwaletea jazba za maisha kila siku wanapojaribu kutumia vibaraste hivyo.

Bw Hassan Awadh, ambaye ni mzee halisi wa kisiwa cha Lamu anafafanua kuwa Lamu si eneo la mbele au Pwani pekee, hasa kwa wale wanaojidai kuujua mji huo.

Bw Awadh anasema tangu jadi Lamu ilitambulika kwa kuwa na mitaa miwili mikuu pekee, ambayo ni Mkomani au kwa jina lingine Utukuni.

Mtaa wa pili uliouunda mji wa kale wa Lamu ni Langoni au kwa jina la jadi Kinooni.

Bw Awadh anashikilia kuwa ni mwenyeji kindakindaki wa Lamu ambaye ameishi mjini humo miaka na mikaka ambaye ana ufahamu wa ndani kuuhusu mji huo wa kihistoria, hivyo kukadiriwa bila hofu kuwa mwenyeji na mjuaji wa mji.

Kulingana na Bw Awadh, mbali na eneo la Pwani au lile la mbele ya mji wa kale wa Lamu na ambalo ndilo linalounda taswira au uso wa Lamu, mji huo wa kihistoria pia umegawanyagawanywa sehemu kadhaa na vichochoro maalum.

“Mbali na eneo hili la mbele la Pwani au mwanzo, mji wa kale wa Lamu pia unajumuisha barabara au kichochoro cha kati kinachojulikana kama ‘Usita wa Mui au Mji.’ Pia kuna sehemu ya ndani ya mji. Hizi sehemu zote ukizizingatia basi hutasumbuka kuizunguka Lamu bila kupotea,” akasema Bw Awadh.

Naye Muhashiam Famau, mzee wa Lamu, anashikilia kuwa endapo huna ufahamu kuihusu mitaa na vichochoro vya mji huo wa kale basi usijidai kuwa unaitambua Lamu.

Anashikilia kuwa zamani, ni mitaa ya Mkomani na Langoni pekee ndiyo iliyounda mji wa kihistoria wa Lamu.

Aidha ujio wa watu wengi umepelekea mitaa mingi kuchipuka mjini, hivyo kuboronga kabisa uhalisia wa mji huo wa kihistoria.

“Kwa mfano, leo utapata mitaa kama Bajuri, Gadeni, Kihobe, Kandahar, Kashmir, Bombay, India, Pakistani, Mararani na kwingineko. Mitaa hiyo yote ilichipuka hivi majuzi tu. Tunavyofahamu kama wazee ni kwamba lazima uwe na ufahamu wa kutosha kuhusu mitaa au vochochoro vya ndani ya mji ndipo tukukadirie kuwa mwenyeji wa Lamu. Iwapo huna ufahamu huo basi wewe bila kutapatapa tutakuita mgeni wa mji,” akasema Bw Famau.

Ikumbukwe kuwa mji wa Kale wa Lamu umedumu kwa zaidi ya miaka 700 na ni miongoni mwa miji ya Ukanda wa Africa Mashariki ambayo wakazi bado wanaishi kwa kufuata mfumo wa zamani wa maisha ambao huonekana na wengi kuwa uliopitwa na wakati.

Ni kwenye mji wa kale wa Lamu ambapo utajiri wa kihistoria umesheheni, ikiwemo kuwepo kwa majumba, misikiti na makaburi ya jadi, vyote vikidumu kwa kati ya miaka 200 na 700.

  • Tags

You can share this post!

MC Jessy adai Gen Z wafurika DM kuomba penzi lake kiujanja

Afcon 2023: Makocha wa timu zilizozembea wafukuzwa kazi

T L