Habari za Kaunti

Joho, usikubali tuhamishwe madini yakichimbwa- Wakazi Kwale

Na SIAGO CECE July 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho anatarajiwa kukabiliwa na changamoto katika wizara aliyoteuliwa ya Madini, huku baadhi ya wakazi wa Kwale wakiingiwa na hofu kutokanana na uchimbaji upya wa madini yanayopatikana katika kaunti hiyo.

Wakazi wa kaunti hiyo wamemwomba Bw Joho aamrishe madini yanayoaminika kuwa na thamani ya mabilioni ya pesa inayopatikana katika eneo la Lungalunga, yasichimbwe.

Wakiongozwa na Richard Onsongo, walisema kuwa kama waziri wa awali, Bw Joho anapaswa kuzingatia hali ya wakazi wa eneo hilo ambao hawataki kuhamishwa ili uchimbaji ufanyike.

“Tunafurahia kwamba ameteuliwa. Tunajua kwamba Kwale ina madini mengi ambayo bado hayajachimbwa, hata hivyo tunataka kumuomba Bw Joho kwamba asijaribu kuchimba madini inayopatikana kwenye milima katika kaunti hii,” Bw Onsongo alisema.

Kulingana na Bw Onsongo, uchimbaji wa Mrima Hill, iliyoko katika Wadi ya Dzombo katika Kaunti Ndogo ya Lungalunga utamaanisha kuwa wakazi kutoka vijiji zaidi ya vitano vinavyozunguka kilima hicho watahamishwa sehemu nyingine.

“Kabla ya chochote, anapaswa kumuuliza gavana wetu Fatuma Achani. Hatuwezi kuruhusu watu wetu kupitia mateso ya kulazimishwa kuondoka katika ardhi yao ya mababu tena,” aliongeza  Bw. Onsongo.

Baadhi ya madini ambayo yangali kuchimbwa Kwale ni ya Niobum, ambayo yanaaminika kuwa na miale ya sumu itakayolaimu wakazi kuhamishwa mbali ili uchimbaji kuendelea.

Haya yanatokea huku wasiwasi ukiendelea kutanda kati ya wakazi wa Kwale kufuatia kufungwa kwa kampuni ya Base Titanium na hatima ya zaidi ya ekari 4000 za ardhi zilizochukuliwa na kampuni kubwa zaidi ya uchimbaji madini katika kaunti hiyo.

Mwasifa Omar, mkazi mwingine, alisema kwamba wanatumaini mawaziri walioteuliwa kutoka kaunti za Mombasa na Kwale watachangia kuleta uwekezaji na maendeleo katika eneo hilo ambalo limekwama kwa muda mrefu licha ya kuwa na rasilimali nyingi.