Kamati yapendekeza Mkongo aondolewe kwa uwaziri Taita Taveta
NA LUCY MKANYIKA
KAMATI ya bunge la kaunti iliyopewa jukumu la kuchunguza sababu za kumwondoa madarakani waziri wa Ardhi Bi Elizabeth Mkongo imependekeza aondolewe afisini.
Hii ni baada ya mwenyekiti wa kamati ya Ardhi wa bunge hilo Bi Hope Anisa kuwasilisha hoja ya kumwondoa madarakani kwa madai ya kutokuwa na uwezo wa kuongoza afisi hiyo na kukiuka maadili.
Hoja hiyo ilimshutumu Bi Mkongo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa na Katiba, Sheria ya Serikali za Kaunti, na Kanuni za Bunge la Kaunti hiyo.
Kamati hiyo teule, iliyoongozwa na mwakilishi wa wadi ya Kasigau Bw Amos Makalo, iliwasilisha ripoti yake mnamo Ijumaa wakati wa kikao maalum, ikisema kuwa ilithibitisha madai 10 kati ya 14 dhidi ya Bi Mkongo.
Kamati hiyo ilipendekeza kuwa bunge hilo la kaunti likubali ripoti hiyo ili kumwondoa Bi Mkongo ofisini kama ilivyopendekezwa na Bi Anisa.
Kamati hiyo iligundua kuwa waziri huyo alikiuka maadili kwa kutumia vibaya ofisi yake, kutumia vibaya rasilimali za umma, kukiuka kiapo cha ofisi, na kukiuka sheria ya uongozi na maadili.
Ripoti hiyo ilisema kuwa Bi Mkongo alishindwa kutimiza wajibu wake wa kupendekeza sera, mapendekezo ya sheria na kanuni za kuongoza serikali ya kaunti katika kusimamia na kulinda ardhi ya umma, sekta za madini na nishati. Pia alishindwa kukamilisha orodha ya thamani ya ardhi ya kaunti, ambayo ni muhimu kwa ukusanyaji wa mapato na mipango ya serikali hiyo.
Kamati hiyo pia ilimshutumu Bi Mkongo kwa kushindwa kutekeleza mipango ya idara hiyo. Pia alishindwa kujibu taarifa zilizowasilishwa kwake na bunge hilo, haswa kuhusu suala la unyakuzi ardhi kati ya wakazi na renchi ya Sagala.
Kamati hiyo ilisema kuwa Bi Mkongo alionyesha ukosefu wa uongozi na kukosa kutoa suluhu za changamoto zinazokabili idara yake, na kushindwa kuhakiki mipaka kati ya ranchi ya Sagala na jamii.
“Waziri wa kaunti alikiri kuwa hakuna mapendekezo ya sheria au sera yaliyowasilishwa kwenye bunge kutoka kwa idara ya Madini,” alisema spika Wisdom Mwamburi aliposoma ripoti hiyo kwenye bunge.
Madai ambayo kamati hiyo haikuthibitisha ni yale ya kucheleweshwa kwa idhini ya mipango ya miji.
Kamati hiyo pia haikupata ushahidi wowote wa kuthibitisha madai kuwa alisimamia uwekaji wa mipaka haramu ya kiwanja huko Voi, au kwamba alipotosha bunge na maafisa wengine kuhusu Afisa Mkuu wa Madini na Nishati anayekaimu.
Bi Mkongo atafika mbele ya Bunge Jumatano wiki ijayo kujibu ripoti ya kamati hiyo, ambayo itawasilishwa kwa majadiliano na kupiga kura.
Kulingana na Kanuni za Bunge la Kaunti, waziri huyo atapewa muda wa saa mbili kujitetea katika kikao cha bunge, baada ya hapo mwenye hoja (Bi Anisa) atajibu na kisha kura kupigwa na wawakilishi hao ili kufanya uamuzi.
Mnamo Alhamisi, waziri huyo alifika mbele ya kamati hiyo na kujitetea dhidi ya madai hayo.
“Sikuja mbele ya bunge kwa sababu nilikuwa nimeenda kupata matibabu. Nina ushahidi wa matibabu yangu ya hospitali,” alisema.
Alisema idara yake pia imekamilisha orodha ya thamani ya ardhi na kuiwasilisha bungeni.