• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Kaunti ya Kilifi yatenga Sh39m kwa basari muhula wa pili

Kaunti ya Kilifi yatenga Sh39m kwa basari muhula wa pili

NA MAUREEN ONGALA

SERIKALI ya Kaunti ya Kilifi imetenga Sh39 milioni kwa basari muhula wa pili.

Serikali ya Gavana Gideon Mung’aro imetangaza kuwa imekamilisha mipango yote ya kurudi shule kwa mamia ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika shule za kitaifa walio katika mpango wa ufadhili wa elimu kutoka kwa serikali hiyo.

Takribani wanafunzi 2,400 wako katika mpango huo.

Akizungumza na Taifa Leo afisini mwake, Waziri ya Elimu wa Kaunti ya Kilifi Felkin Kaingu alisema kuwa serikali imetenga Sh39 milioni kuwalipia karo wanafunzi hao katika muhula huu wa pili.

“Ningependa kuwajulisha wazazi na wakazi wote wa Kilifi kuwa ufadhili wa wanafunzi wote wa shule za kitaifa uko imara na tayari tumetenga Sh39 milioni kuwalipia wanafunzi hao. Tumejipanga kuhakikisha ya kwamba watoto wetu wanaenda shuleni bila changamoto,” akasema Bw Kaingu.

Alisema kuwa bodi ya ufadhili ya Kaunti ya Kilifi ilipokea pesa hizo Jumanne na tayari maafisa wanaandika hundi kwa shule mbalimbali.

Alisema tofauti na awamu ya kwanza ya mpango huo, bodi inayosimamia ufadhili huo itaandika hundi mojamoja kwa shule na sio kwa afisi za wawakilishi wadi.

“Kufikia Ijumaa (leo) tutakuwa tumeandika hundi zote kwa shule za kitaifa 35,” akasema.

Waziri huyo alisema kuwa serikali ya kaunti imepiga hatua kubwa kutatua changamoto ambayo ilijitokeza ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wanalipiwa karo na zaidi ya mfadhili mmoja.

Pia baadhi yao walikuwa wamepata ufadhili kutoka kwa zaidi ya wadi moja.

Kupitia hatua hiyo, idadi ya wanafunzi katika ufadhili wa kaunti ya Kilifi imepungua kutoka 2,900 katika muhula wa kwanza hadi 2,400 muhula huu.

“Tumerekebisha tatizo hilo na hakuna mwanafunzi amelipiwa karo zaidi ya mara moja. Kufikia sasa wanafunzi ambao tuko nao katika orodha yetu ni wale ambao hawajapata ufadhili wowote kutoka kwa wahisani ama mashirika na benki,” akaeleza.

Alisema kwa sasa wanalenga kutumia muundo wa kisasa ambao utasaidia kutatua changamoto hiyo katika siku za usoni kwani itaonekana mara moja iwapo mwanafunzi yuko katika ufadhili huo na amelipiwa karo zaidi ya mara moja.

Alisema kuwa mipango ya kuimarisha miundomsingi katika shule za mashinani italenga pia kuanzishwa kwa miradi kadhaa ya maendeleo katika miji ya Kilifi ambapo kuna kiwango kikubwa ya umaskini.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

DPP apinga mfungwa wa ugaidi kukaa jela siku nane tu!

Mvurya awavulia kofia kina mama Pwani kwa bidii yao kiuchumi

T L