Habari za Kaunti

Kaunti ya Nairobi yanunua fimbo ya Sh33 milioni wafanyakazi wakila hu

Na WINNIE ONYANDO September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa wengi katika bunge la Kaunti ya Nairobi, Peter Imwatok amesema kuwa wanahitaji ulinzi wa ziada baada ya bunge hilo kununua mesi yenye thamani ya zaidi ya Sh30 milioni.

Akizungumza Jumanne Septemba 10,2024 baada ya fimbo hiyo ya kuashiria mamlaka kukabidhiwa spika wa kaunti hiyo, Bw Imwatok alisema kuwa wasingetaka mesi hiyo ya thamani kubwa iibwe kama ilivyotokea hapo nyuma.

“Baada ya kutumia kiasi hicho cha pesa kununua fimbo ya mamlaka ya kaunti, tunahitaji ulinzi sasa Bw Spika. Hatutaki kilichotokea hapo nyuma ijitokeze tena,” akasema Bw Imwatok.

Kando na hayo, alisema kuwa fimbo hiyo imetengenezwa kwa vipande vya dhahabu ya karati 11.

Mnamo Januari 2024, serikali ya kaunti ya Nairobi ilialika mashirika mbalimbali ya kuunda na kusambaza mesi kutuma maombi ya kupewa zabuni hiyo.

Kaunti ya Nairobi ilisema kuwa fimbo hiyo kuanzia kichwa hadi mkia ingekuwa na sehemu ya dhahabu yenye karati 18.

Uzito wa jumla wa fimbo ulipangwa kuwa kati ya kilo 10 hadi kilo 10.5 wakati urefu ulitakiwa kuwa karibu mita 1.2.

Kando na hayo, lilikusudiwa kugawanywa vipande sita, kila kipande kingetengenezwa kwa shaba na kupakwa madini ya fedha.

Haya yanajiri huku mamia ya wafanyakazi katika kaunti hiyo wakikosa mishahara na marupurupu kwa muda sasa.