Habari za Kaunti

Kaunti yalemewa na ongezeko la visa vya Kalazaar hospitali zikijaa

Na JACOB WALTER March 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya Kaunti ya Wajir imezidiwa na ongezeko la idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Kalazaar huku hospitali zikijaa hadi pomoni.

Ugonjwa huo pia umesababisha vifo tisa kufikia sasa.

Afisa Mkuu wa Huduma za Matibabu Mohammed Guhad alisema vituo vya afya vimelemewa na ongezeko la maambukizi tangu ugonjwa huo ulipozuka Septemba 2024.

“Kufikia sasa tumepoteza watoto tisa walio na umri wa chini ya miaka mitano. Wengi wao wanatoka maeneobunge ya Eldas na Wajir Magharibi,” Bw Guhad alisema.

Watoto waathirika zaidi

Kituo cha afya cha Eldas kinaongoza kwa idadi ya juu zaidi ya wagonjwa 150 huku Arbajan kikiwa na 130.

Zaidi ya hayo, asilimia 84 ya wagonjwa katika vituo mbalimbali vya afya kwenye kaunti hiyo ni watoto walio chini ya miaka mitano, ikilinganishwa na asilimia 0.4 ya wagonjwa walio kati ya miaka 30-40.

Kitengo cha ugatuzi kilikuwa kimetenga wodi za ziada katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Wajir ili kustahimili ongezeko la wagonjwa kutoka Wajir Kaskazini, Bw Guhad alieleza.

Mnamo Jumanne, Gavana Ahmed Abdullahi wa Wajir alitoa wito kwa wakazi na wadau wa afya kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.