• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kaunti yaondoa marufuku ya kutumia fuo baada ya Hidaya kudhoofika

Kaunti yaondoa marufuku ya kutumia fuo baada ya Hidaya kudhoofika

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeondoa marufuku dhidi ya uogeleaji katika fuo zake.

Waziri wa Utalii na Biashara, Bw Mohamed Osman, alisema marufuku hayo yameondolewa baada ya tishio la kimbunga Hidaya kuisha.

Hata hivyo Bw Osman aliwaonya wakazi na watalii wanaopanga kuzuru fuo za Mombasa kuwa waangalifu mvua ikiendelea kunyesha eneo la Pwani na upepo mkali kushuhudiwa.

“Tunawasihi watu wawe makini wanapoenda kuogelea kwa sababu bado hali ya hewa si nzuri, kuna upepo mkali na mvua ingali inanyesha,” alisema Bw Osman.

Mnamo Jumamosi, Gavana Abdulswamad Nassir alipiga marufuku uogeleaji na kujinvinjari baharini akisema ni hatua za tahadhari katika kukabiliana na athari zilizotarajiwa za Kimbunga Hidaya.

Vilevile alisimamisha shughuli zote za ujenzi, matembezi katika fuo na uvuvi baharini.

Bw Nassir aliagiza maafisa wa Kaunti, washirikiane na Polisi wa Kitaifa, Jeshi la Wanamaji la Kenya, na Kikosi cha Coast Guard, kuhakikisha utekelezaji wa agizo la kutoingia katika Bahari Hindi kwa wakazi hadi kimbunga kipite.

Aidha, aliwaomba mameneja wa hoteli kuchukua jukumu la kukataza wageni dhidi ya kutumia bahari hadi ukaguzi ufanywe upya usiku wa Jumatatu.

Gavana Nassir alisisitiza umuhimu wa hatua za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kufunga visima na vidimbwi vya maji pamoja na kuimarisha miundo ya paa.

  • Tags

You can share this post!

Trump sasa ahusishwa moja kwa moja na ponografia

MAONI: Bunge lina uwezo wa kuokoa Kenya kwa kuchangia...

T L