Kaunti yatetea hatua ya kukodisha mitambo ya kukarabati barabara
SERIKALI ya Kaunti ya Kajiado imetetea mpango wake wa kukodisha mitambo ya ukarabati wa kawaida wa miundombinu ya barabara, badala ya kununua vifaa hivyo moja kwa moja vimilikiwe na kaunti.
Waziri wa Fedha wa Kaunti, Alais Kisota, pamoja na mwenzake wa Barabara, Kazi za Umma na Uchukuzi, Dkt Jackton Achola, waliambia Bunge la Kaunti kwamba gharama ya kukodisha na kununua “haiwezi hata kulinganishwa.”
Walipofika mbele ya Kamati ya Bunge nyakati tofauti, mawaziri hao walifafanua kuwa bajeti ya ununuzi wa magari ya kaunti ni tofauti na bajeti ya kukodisha mitambo kwa ukarabati wa kawaida wa barabara.
Bw Kisota alisema kaunti imetenga Sh165 milioni 165 kukodisha matingatinga kwa ukarabati wa barabara katika kaunti nzima. Kiasi hiki kinasaidia bajeti ya Sh350 milioni ambayo tayari ilitengwa kwa ujenzi wa barabara, vivukio na madaraja. Matingatinga hayo tayari yamesambazwa katika maeneo matano ya ubunge kufanya kazi katika barabara tatu katika kila wadi 25.
Dkt Achola alisema serikali iliamua kutumia makubaliano ya kukodisha baina ya serikali (G2G) na Idara ya Huduma za Mitambo na Uchukuzi ya Serikali Kuu kwa sababu ni mkataba wa haki zaidi kwa “gharama, ufanisi na utekelezaji wa kazi kwa wakati.”
Bw Kisota alisisitiza kuwa kununua vifaa vyote vinavyohitajika, kuvidumisha na kuhakikisha vinatumika kwa kutegemewa katika barabara zote zilizopangwa, ni ghali sana na halitekelezeki kwa uhakika.
“Ukikodisha, unatatua suala zima la ukarabati , madereva na mafuta. Tunachohitaji ni kutoa ratiba ya kazi kwa mkodishaji,” Kisota aliwaambia madiwani.
Aliongeza kuwa ununuzi wa baadhi ya magari mapya kwa matumizi ya kaunti ulitengewa bajeti na kuidhinishwa na bunge ili kuboresha utoaji wa huduma katika idara mbalimbali.
“Utaona kuwa magari mengi ya kaunti ni ya zamani sana, mengine yameharibika, mengine ni ya zamani na hayafai tena kutumika,” alisema.
“Hakuna serikali inayoweza kuendesha shughuli zake kwa ufanisi bila kuwezesha usafiri wa maafisa wake,” aliongeza Kisota.
Awali, kulikuwa na ripoti kuwa baadhi ya madiwani walionyesha wasiwasi kuhusu mpango huo wakihofia kwamba utachelewesha ujenzi wa barabara katika kaunti.
Lakini Bw Kisota alibainisha kuwa barabara ambazo tayari zimekabidhiwa kwa wakandarasi zitaendelea kujengwa.
“Barabara nyingi ambazo tunapeleka mitambo ni zile zinazofungua maeneo mapya au ambazo hazikutengewa fedha. Baadhi ni zile zilizoharibiwa na mvua na zingechukua muda mrefu kutengewa bajeti,” alisema.