Kinaya uhalifu ukizidi kwa Gachagua, Wakuu wa Polisi na Majeshi
ENEO bunge la Mathira katika kaunti ya Nyeri, anakotoka Naibu Rais Rigathi Gachagua, ni mojawapo ya maeneo yanayokabiliwa na ukosefu wa usalama.
Hii ni kinaya kwani eneo hilo lina idadi kubwa ya polisi na pia lina vituo sita vya polisi.
Eneo hilo limeripoti visa vingi vya uhalifu katika wiki za hivi karibuni, jambo ambalo linashangaza.
Wakazi na wanachama wa jumuiya ya wafanyabiashara katika mji huo, walisema kuwa wanatarajia eneo hilo kuwa mojawapo ya maeneo salama zaidi nchini hasa kwa kuwa Naibu Rais anatoka hapo.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) mteule Bw Douglas Kanja na Mkuu wa Majeshi Charles Kahariri, pia wanatoka katika eneo hilo.
Bw Kanja amekuwa akihudumu kama naibu wa Inspekta Jenerali wa Polisi na ambaye hapo awali alikuwa kamanda wa Kitengo cha GSU.
Katika muda wa wiki mbili, maduka makubwa mawili ya vifaa vya elektroniki yamevamiwa usiku huku wananchi wakitilia shaka utendakazi wa polisi wanaoshika doria usiku.
Matukio kadhaa ya wizi wa mabavu pia yameripotiwa katika eneo hilo.
Wakazi hao walisema vurugu wakati wa uvamizi huo zilisikika kutoka mbali, ikiwa ni pamoja na kituo cha polisi cha Karatina ambacho kiko umbali wa mita 300.
“Tunaishi kwa hofu ya kushambuliwa na hapa si salama tena kwani hujui ni lini unaweza kuvamiwa. Serikali inafaa kuchukua hatua za haraka,” akasema Bw Patrick Kariuki Kiruthu ambaye ni mhudumu wa duka la kutengeneza vifaa vya ujenzi.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Mathira Mashariki, Bw Samson Leweri , alisema hadi sasa polisi bado hawajamkamata mtu yeyote kuhusiana na hali ya ukosefu wa usalama ya hivi karibuni lakini alithibitisha kuwa wafanyabiashara hao walikutana na maafisa wa usalama ambapo walielezea wasiwasi wao.
“Tunaendelea na uchunguzi na ninawahakikishia wakazi kwamba tutafikia mwisho wa hili,” alisema.
Mwezi uliopita, kamishna wa Kaunti ya Nyeri, Bw Pius Murugu aliambia wanahabari kwamba Mathira inachukuliwa kuwa eneo ‘la kipekee’ kwa sababu ni nyumbani kwa naibu Rais.
Miezi miwili iliyopita Bw Benjamin Boen aliwekwa katika eneo hilo lakini akahamishwa hadi kaunti ya Lamu ambako yeye ni naibu kamanda wa kaunti.