Kindiki aonya polisi wanaoshirikiana na wahalifu
NA DAVID MUCHUI
WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, ameapa kuchukua hatua kali dhidi ya polisi wanaoshirikiana na wahalifu kuwaruhusu kuendesha uhalifu bila kuwakabili.
Hili linafuatia ongezeko la visa vya wizi wa ng’ombe katika Kaunti ya Meru.
Akiwahutubia maafisa wa usalama katika kaunti za Meru na Laikipia mnamo Jumamosi, Machi 2, 2024 Prof Kindiki alieleza wasiwasi wake kwamba baadhi ya polisi na maafisa wa utawala wamekuwa wakipokea hongo kutoka kwa wahalifu, ili kuwaruhusu kuendeleza uhalifu bila kuwachukulia hatua zozote.
“Unafaa kupatia kipaumbele eneo lolote linalokabiliwa na wizi wa ng’ombe. Kwa wiki mbili zilizopita, kumekuwa na msururu wa visa vya uvamizi. Hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea tena. Tutakabiliana na polisi yeyote ambaye ni sehemu ya tatizo hilo,” akaonya Prof Kindiki.
Kauli yake ilijiri siku chache baada ya baadhi ya wabunge kutoka Meru kushinikiza serikali kuwahamisha maafisa wa polisi wa ngazi za juu katika kaunti hiyo, kutokana na ongezeko la visa vya wizi wa ng’ombe.
Baadhi ya wabunge hao ni Dan Kiili (Igembe ya Kati), Joseph Taitumu (Igembe Kaskazini), Mpuru Aburi (Tigania Mashariki), Moses Kirima (Imenti ya Kati), JohnPaul Mwirigi (Igembe Kusini), John Mutunga (Tigania Magharibi), Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Shadrack Mwiti (Imenti Kusini).
Walisema kuwa ongezeko la wizi wa ngo’mbe umewaacha wachungaji wengi wakiwa maskini.