Habari za Kaunti

Kitendawili MCA akipigwa risasi mjini

Na DAVID MUCHUI March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWAKILISHI wa Wadi (MCA)  ya Burat katika Kaunti ya Isiolo, Bw Nicholas Lorot, amelazwa hospitalini baada ya kupigwa risasi  mjini Isiolo Jumatano usiku.

Kamishna wa Kaunti ya Isiolo, Bw Geoffrey Omoding, alisema MCA huyo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Kiirua huko Meru, hayuko hatarini.

Inadaiwa kuwa MCA huyo alikuwa akiendesha gari karibu na hoteli ya Northern Galaxy wakati mshambuliaji aliyekuwa peke yake  alipotoa bunduki na kumfyatulia risasi kadhaa.

“MCA alikuwa mwepesi na alijificha ili kuepuka majeraha mabaya. Alipigwa risasi begani na mkononi kisha akakimbizwa hospitalini,” alisema Bw Omoding.

Aliongeza kuwa, “Polisi wanachunguza kwa nini mshambuliaji huyo alimlenga MCA na pia wanachunguza picha za CCTV kutoka eneo hilo ili kupata ushahidi kuhusu mshukiwa huyo asiyejulikana.”

Mwaka jana, Bw Lorot alikuwa mkosoaji mkali wa utawala wa kaunti kabla ya kunyamaza huku kukiwa na ripoti kwamba alikuwa amepatana na Gavana Abdi Guyo.

Mnamo Novemba mwaka jana, MCA huyo alidai kuwa alipokea jumbe za vitisho wakati wa kilele cha ukosoaji wake dhidi ya utawala wa kaunti.

Bunge la Kaunti lililaani tukio hilo la ufyatuaji risasi na kuitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina.

Katika taarifa yake, Spika Mohamed Roba Qoto alisema Naibu Spika David Lemantile alikabidhiwa jukumu la kusalia hospitalini kutoa msaada kwa MCA aliyejeruhiwa.

“Tumejizatiti kuhakikisha amani, usalama, na haki kwa wakazi wote. Tunashirikiana kwa karibu na idara za usalama ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa,” ilisema taarifa ya Bunge la Kaunti.