Kitendawili mwanaume akifa gerezani siku mbili baada ya kuzuiliwa
MWANAUME mwenye umri wa miaka 28 aliaga dunia siku mbili baada ya kuzuiliwa katika Gereza la Nakuru kwa kushindwa kulipa dhamana ya pesa taslimu.
Dennis Kiprotich, makanga wa matatu, alikamatwa mnamo Machi 21 na maafisa waliovaa kama raia baada ya makabiliano na abiria katika eneo la mji wa Nakuru.
Kisha alipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nakuru ambako alizuiwa wikendi kabla ya kufikishwa mahakamani Machi 25 na kukanusha mashtaka ya kushambulia na kumjeruhi abiria kinyume na kifungu 251 cha Kanuni ya Adhabu.
Maelezo katika karatasi ya mashtaka yalionyesha kuwa mnamo Februari 28 Nakuru Mashariki, Kiprotich alimvamia na kumjeruhi Stanley Kibuku Njoroge.
Kiprotich alikana mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh10, 000 na mdhamini sawa na hilo lakini akakosa kuongeza kiasi hicho.
Alizuiliwa katika Gereza la Nakuru GK ambapo alifariki baadaye katika hali isiyoeleweka.
Kesi yake ilipangwa kutajwa Aprili 7.
Familia yake, makanga wenzake na wanaharakati wa haki za binadamu sasa wanadai majibu wakitaja majeraha yanayoonekana kwenye mwili wake na ukosefu wa mawasiliano sahihi kuhusu hali yake akiwa kizuizini.
Kulingana na dadake mkubwa Judith Chebet, mwathiriwa alimpigia simu Machi 25 akiwa amefadhaika na kutafuta usaidizi wa kuchangisha Sh3, 000 ili aachiliwe.
Mama yao alituma pesa hizo na saa moja baadaye, alipiga simu tena, safari hii akisema anahitaji Sh10, 000 au apelekwe gerezani.