Habari za Kaunti

Kizaazaa bodaboda aliyetorosha dada wawili ‘kichipsi funga’ akikamatwa

May 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA GEORGE MUNENE

MWENDESHAJI bodaboda anayedaiwa kuwatorosha dada wawili na kukaa nao ‘kichipsi funga’ kwa muda wa mwezi mmoja, amekamatwa na polisi katika Kaunti ya Kirinyaga.

Polisi walivamia nyumba ya kupanga ya mshukiwa katika kijiji cha Kimandi mnamo Ijumaa jioni na kuwaokoa akina dada hao ambao ni wanafunzi wa shule za upili na kumkamata mshukiwa.

Mshukiwa mara baada ya kukamatwa alipelekwa hadi kituo cha polisi cha Kerugoya kuhojiwa huku dada hao wakipelekwa hospitalini kuchunguzwa.

Kulingana na familia ya waathiriwa, bodaboda huyo aliwapumbaza wasichana hao na kuwachukua.

Kisha akawafungia katika chumba cha kupanga na inadaiwa amekuwa akiwanyanyasa kingono.

“Wasichana wangu walipotea katika hali isiyoeleweka na hii ilitutia wasiwasi mno,” baba ya wasichana hao akasema.

Baba huyo alisimulia jinsi familia hiyo ilivyoanza msako mkali wa kuwatafuta wasichana hao na kuripoti kisa hicho kwa polisi.

“Nilifanya uchunguzi wangu kwa muda wa mwezi mzima na kubaini kuwa binti zangu walikuwa wanashikiliwa na mhudumu huyo ambaye anafahamika sana kijijini. Baadaye nilimfahamisha naibu chifu na polisi ambao walivamia nyumba yake na kumpata mshukiwa akiwa na binti zangu,” akaeleza.

Alisema mmoja wa wasichana hao ni mwanafunzi wa Kidato cha Tatu na mwingine ni wa Kidato cha Nne.

“Bodaboda huyo ameharibu maisha ya binti zangu na sasa ninalilia haki… mhudumu ni sharti aadhibiwe,” akasema mzazi huyo.

Jambo la kushangaza ni kwamba, baba huyo alisema hata surupwenye yake ya kazi, vitambulisho na stakabadhi nyingine za kibinafsi, zilipatikana nyumbani kwa mshukiwa.

Kizaazaa kilizuka wakati wa kukamatwa kwa mshukiwa ambapo wanakijiji waliojawa na hasira nusra wachukue sheria mkononi.

Hata hivyo, polisi waliuzuia umati huo, wakamwingiza mshukiwa kwenye gari la serikali.

Mkuu wa polisi katika Kaunti Ndogo huko Kirinyaga, Bw John Torori, alisema mshukiwa atafikishwa mahakamani mara tu uchunguzi utakapokamilika.

Aliiomba familia na wakazi kuwa na subira, huku akiwahakikishia kuwa mshukiwa bila shaka atakabiliwa na mkono wa sheria.

Wakazi walidai bodaboda huyo anajulikana kwa tabia chwara na hapaswi kuachwa.

“Amekuwa akiharibu maisha ya wasichana wa shule katika kijiji hiki kwa muda mrefu na anapaswa kufungwa… hatutaki arudi kijijini hapa,” mkazi mmoja akasema.