Knut yapendekeza walimu Baringo wajihami kwa silaha kukabili majangili
NA FLORAH KOECH
CHAMA cha Kitaifa cha Walimu nchini Kenya (Knut), sasa kinawataka walimu katika maeneo yanayokabiliwa na visa vya ujangili katika Kaunti ya Baringo waruhusiwe kujihami kutokana na ukosefu wa usalama unaoendelea.
Tawi la Knut katika kaunti hiyo, limeiomba serikali kuwaruhusu walimu kujihami kwa kuwa hawajahakikishiwa usalama wao.
Hayo yanajiri baada ya mauaji ya naibu mwalimu mkuu kutoka mpakani mwa shule ya msingi ya Tuluk katika eneo la Baringo Kaskazini, ambaye alipatikana amekufa akiwa na majeraha ya risasi Jumapili asubuhi.
Kisa hicho kilitokea mita chache kutoka kituo cha biashara cha Tuluk kufuatia shambulio linaloshukiwa kutekelezwa na majangili.
Wenyeji walisema mwalimu wa shule ya msingi, Bw Elijah Simotwo, 57, alionekana mara ya mwisho kwenye kituo cha biashara siku ya Jumamosi mwendo wa saa nne za usiku.
Kamanda wa Polisi kaunti ya Baringo, Bw Julius Kiragu, alisema mwili wa mwalimu huyo ulipatikana asubuhi ukiwa na majeraha ya risasi kifuani.
“Mazingira ambayo mwalimu huyo aliuawa hayajabainika. Wenyeji wanadai kuwa alionekana mara ya mwisho katika kituo cha biashara saa nne za usiku. Bado tunachunguza kujua ni nini kilisababisha na ni nani alihusika katika uhalifu huo,” Bw Kiragu alisema.
Mauaji ya mwalimu huyo yamefikisha sita idadi ya watu waliouawa katika eneo hilo kwa muda wa siku tano.
Visa vya mashambulio ya majangili katika vijiji vinavyokabiliwa na ukosefu wa usalama vinaendelea hata baada ya serikali kuanzisha operesheni ya Maliza Uhalifu North Rift.
Katika operesheni hiyo, walinda usalama waliwapokonya silaha na kuwafukuza wahalifu waliojihami mwaka jana.
“Vitu pekee vinavyobebwa na walimu ni kalamu na vitabu. Ikiwa hawajahakikishiwa usalama wao, basi waruhusiwe kumiliki bunduki ili kujilinda,” Katibu Mtendaji wa Knut, Askofu Joshua Cheptarus, akasema.
Alisema chama hicho kitawakusanya walimu ukanda huo kufanya maandamano hadi silaha zote haramu zilizoko mikononi mwa raia zitakapotwaliwa iwapo serikali haitafanya lolote kurejesha utulivu katika maeneo yenye matatizo.
“Tunawaomba walimu katika shule zinazokabiliwa na ujangili katika eneo hili ambao wanahisi kutokuwa na usalama waripoti kwa Wizara ya Elimu kwa sababu hatutaki kupoteza mwalimu mwingine yeyote kwa ujangili tena,” mwanaharakati huyo akasema.
Chama cha walimu kimelaani mashambulio ya mara kwa mara katika eneo hilo kutokana na kumilikiwa kwa bunduki haramu.
Knut ina wasiwasi kuwa hali hiyo imelemaza masomo na maendeleo katika maeneo yaliyoathiriwa.
Afisa huyo wa Knut alisema taasisi za masomo zinafaa kuwa mahali salama kwa wanafunzi wote, ilhali leo hii ni walengwa wa majangili wenye silaha, na kusababisha wengi wao kuhama na kiwewe miongoni mwa watoto.
Mauaji ya mwalimu huyo yamezua hali ya wasiwasi katika vijiji vinavyokabiliwa na ujangili, huku wenyeji wakidai kuwa hawawezi kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa kuwa wanahofia wahalifu wenye silaha wanazurura vijijini bila kukamatwa.