Habari za Kaunti

Kunguru wanavyonyang’anya watalii chakula Diani na kuwa kero kwa wakazi

Na SIAGO CECE September 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa Diani, Kaunti ya Kwale, wamelazimika kutafuta msaada wa wafadhili ili kuondoa ndege aina ya kunguru ambao wamekuwa kero kubwa kwa jamii.

Inasemekana kuwa ndege hao waliingia nchini miaka ya 1940, lakini ongezeko la idadi yao limewaletea wakazi kero kubwa, hasa wanapovamia chakula moja kwa moja kutoka kwa wageni katika hoteli za kitalii.

“Ndege hawa ni tishio sio tu kwa utalii, bali pia kwa mazingira yetu. Kazi hii ilipaswa kufanywa na Shirika la Wanyamapori Kenya (KWS), lakini wamechukua muda mrefu,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wakazi wa Pwani ya Kusini (SCRA), George Mokaya.

SCRA imeeleza kuwa kunguru hao hubeba magonjwa yasiyopungua manane, na hivyo kuwaweka watu katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo. 

Pia, kunguru hao wanachafua maeneo kwa kinyesi chao wanapokaa chini ya miti au popote wanaposimama. 

Mbali na hayo, wameshambulia ndege wengine kwa kuharibu viota na kula mayai yao.

Chama hicho kimeomba wafadhili kuwasaidia kupata sumu maalum iitwayo Starlicide, ambayo imeundwa kuua kunguru.

Wamesema kuwa wanahitaji Sh20 milioni ili kununua sumu hiyo.

“Tunahitaji fedha kununua kemikali ya Starlicide. Tukipata fedha hizo, tutapata sumu hiyo ifikapo mwisho wa Oktoba,” ilisoma sehemu ya barua hiyo.

Walieleza kuwa utengenezaji wa sumu hiyo huchukua kati ya wiki nne hadi sita, na kusafirisha inachukua takriban wiki mbili. 

Ikiwa hawatapata fedha kufikia muda huo, wataipata mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Kufikia sasa, wamekusanya sh 3.5 milioni, lakini wanatarajia kukusanya Sh15 milioni kupitia michango.

Hata hivyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imesema kuwa SCRA lazima ifanye tathmini ya mazingira kabla ya kuidhinisha kutumia sumu hiyo kuwauwa ndege hao.

Simu hiyo inatarajia kutumia saa 12 kuwaua ndege baada ya yao kuila.

Mkurugenzi wa NEMA Kaunti ya Kwale Bw Duncan Okoth, alisema kuwa sumu hiyo inaweza kuwa hatari kwa maji au mazingira ikiwa haitadhibitiwa ipasavyo. 

Kwa sasa alisema afisi hiyo ingali kupokea ripoti hiyo.