Habari za Kaunti

KWS yatoa ilani baada ya plastiki kuua nyangumi Kwale

Na WINNIE ATIENO December 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHIRIKA la Kuhifadhi Wanyamapori nchini (KWS) limeonya Wakenya dhidi ya kutumia plastiki katika sehemu za ufuoni ili kuzuia kuhatarisha maisha ya wanyama wa baharini.

Hii ni baada ya nyangumi aliyepatikana ameangamia karibu na ufuo wa Leopards katika Kaunti ya Kwale hivi majuzi, kuthibitishwa alisakamwa na chombo cha plastiki utumboni.

KWS ilisema daktari wa mifugo, Dkt Asuka Takita, alifanya uchunguzi wa mzoga huo na kugundua nyangumi hakufa kwa hali ya kawaida bali kutokana na uchafuzi wa mazingira.

“Nyangumi ambaye ni mnyama mpole sana alifariki dunia kutokana na uharibifu wa mazingira yetu baharini. Upasuaji ulionyesha chombo cha plastiki kilichokwama kwenye utumbo wake,” KWS ilisema.

Kwenye taarifa kupitia mtandao wa kijamii, KWS ilionya Wakenya kuhusu taka za plastiki zilizosheneni baharini na kuhatarisha maisha ya wanyama wa baharini.

“Taka za plastiki zilizosheheni baharini kwa miaka, zinaendelea kuhatarisha maisha ya wanyama wa baharini na hata kusababisha vifo vya samaki. Tuache kuharibu mazingira,” KWS iliongeza.

Kenya ilipiga marufuku utumizi wa chupa za plastiki mnamo Juni 2020 katika maeneo yaliyohifadhiwa kama vile mbuga za kitaifa, misitu, na fukwe.

Sheria hii inawazuia wageni kuingiza plastiki hizo ndani ya maeneo hayo.

Hata hivyo, plastiki zinaendelea kutumika katika baadhi ya hoteli za kifahari zinazopakana na fuo za bahari, hasa wakati wa makongamano.

KWS ilisema taka za plastiki baharini hukaa kwa miaka mingi, zikielea na kuzama kupitia mifumo ya ikolojia ya baharini ambapo hudhuru na kuua viumbe wa baharini.

Hasara hii inadhihirisha hatari kubwa ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na binadamu.

Tunapotazamia mwaka mpya, KWS iliwasihi Wakenya kuwajibika na kuacha kutupa taka ovyo baharini.