Magenge ya unyakuzi wa ardhi yazidi kutikisa jiji la Eldoret
MAGENGE ya unyakuzi wa ardhi na mali nyingine jijini Eldoret yanaendelea kutumia hati ghushi za ardhi kufurusha familia kutoka kwa mali yao.
Tukio la hivi karibuni ni la kina dada wawili, Bi Julia Chepkoech Gimnyigei na Esther Cherotich Gimunyigei ambao wanaomba serikali kuchukua hatua dhidi ya mtandao wa genge hilo ambalo linaendeleza ufisadi wa ardhi kwa ushirikiano na baadhi ya mawakili walaghai na wanasiasa katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Katika hati yao ya kiapo walidai kuwa makundi yenye nguvu yameifanya familia yao kukosa makao na kukosa ardhi kwa kunyakua ardhi yao katika eneo la Kapsaret kwa kutumia vyeti ghushi.
Wanadai kundi hilo, linalofanya kazi kwa kushirikiana na maafisa wa ardhi limeacha familia ya ndugu wanane bila ardhi.
Mahakama inatarajiwa kutoa mwelekeo wa ombi lao mnamo Desemba 16.
Matukio kama hayo yanazidi kuongezeka kupitia kwa kampuni zinazouza ardhi na kuacha familia nyingi hohe hahe bila ardhi jijini humo.
Kesi kama hizo zimekuwepo katika mahakama za Eldoret kwa muda mrefu.
Mara kwa mara Mahakama ya Mazingira na Ardhi (ELC) hukabiliana na kesi za ulaghai, ugawaji wa ardhi kinyume cha sheria na umiliki bandia ambao husababisha kuhamishwa kwa wamiliki halali wa ardhi husika.
Kesi kadhaa mashuhuri kutoka kwa ELC, Eldoret zinaangazia ukubwa wa tatizo, ambapo mizozo ya ardhi inayohusishwa na mabroka na maafisa wasio waaminifu imesababisha familia kukabiliwa na madhara makubwa.
Mnamo mwaka wa 2020 Mahakama ya Ardhi na Mazingira ya Eldoret iliamrisha fidia ya Sh4.5 bilioni kulipwa familia za Joseph arap Korir na Kiptot arap Sitienei kwa kupoteza ekari 1,050 za ardhi yao ambayo sasa ndio kuna mtaa wa mabanda wa Langas.
Wakati wa uamuzi huo Jaji Anthony Ombwayo alikiri kwamba ardhi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mamia ya familia zilizonunua mashamba kupitia ‘mabroka kwa ushirikiano na maafisa’ wa lililokuwa baraza la manispaa ya Eldoret.
Kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu mjini Eldoret, kesi hzo zinaonyesha namna ulaghai umekithiri katika sekta ya ardhi jijini humo.
Kimutai Kirui kutoka Centre Against Torture alisema mahakama inahitaji kuwa makini na kutoa nafasi kwa pande zote kusikilizwa na hata kuzuru ardhi inayozozaniwa ili kupata taarifa sahihi kutoka mashinani.
‘Baadhi ya wamiliki halali wa ardhi wanapoteza ardhi yao kwa sababu ya kutojua kusoma na kuandika, mahakama inahitaji kufanya kwa makini sana kabla ya kutoa maamuzi haswa kwa familia ambazo zimo hatarini kwenye mzozo wa mali na ardhi,’ alisema Bw Kirui.
Mojawapo ya kesi ambayo inaendelea mahakamani humo ni kesi ambapo mwalimu wa shule ya upili ni miongoni mwa watu watatu walioshtakiwa kwa kula njama ya kulaghai na kujipatia mali ya zaidi ya Sh10 milioni kutoka kwa mkulima wa Eldoret.
Katika kesi hiyo, Mark Kibet Kibii, mwalimu wa shule ya upili kutoka Nakuru, Samson Chumba, na Sophie Jepkemei Keitany, walishtakiwa mbele ya mahakama ya Eldoret kwa kula njama ya kumlaghai John Bor shamba na nyumba yake iliyoko Cheplaskei katika Kaunti Ndogo ya Kesses.
Uchunguzi wa awali wa makachero kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai umebaini kuwa stakabadhi zilizotumika katika shughuli hiyo ni bandia.
Hakimu Mkuu Mwandamizi Kimani Mukabi aliwaachilia washukiwa kwa dhamana ya Sh500,000 au dhamana ya pesa taslimu ya Sh200,000.
Mahakama imewazuia kujishughulisha na mali hiyo hadi kesi isikizwe na kuamualiwa. Kesi hiyo itaanza kusikilziwa mnamo Februari 2, 2026.