Habari za Kaunti

Mahakama yaambiwa ‘ada fiche’ ndizo zilitatiza mpango wa masomo Finland

Na JOSEPH OPENDA July 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SHAHIDI katika kesi ya sakata ya Sh1.1 bilioni ya ufadhili wa masomo nchini Finland inayomkabili Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago alifichulia mahakama ya Nakuru kwamba ada zilizofichwa zilitatiza mpango huo.

Ada za ziada zilifanya vigumu kwa wanafunzi kuendelea na masomo yao huku wazazi wakihangaika kulipia gharama zisizotarajiwa.

Bi Salina Cherono, afisa wa kaunti ambaye mwanawe alipata ufadhili wa masomo, alitoa ushahidi kwamba alichukua mkopo wa Sh918,000 alizolipa katika Hazina ya Masomo ya kaunti ya Uasin Gishu.

Mwanawe, ambaye alipaswa kusomea uuguzi katika Chuo Kikuu cha Laurea nchini Finland, alilazimika kukamilisha kozi ya miezi mitatu katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Rift Valley huko Eldoret, ambayo ilijumuisha lugha ya inayozungumzwa Finland.

“Mwanangu pamoja na wengine walifundishwa lugha ya Finland pamoja na ujuzi mwingine ili kuhakikisha masomo yake nchini Finland yangekuwa sawa,” alisema Bi Cherono.

Cherono baadaye alitakiwa kulipa Sh160,000 za ziada kwa gharama ya viza na bima, jambo ambalo alifanya mnamo Mei 17.

Baada ya kungoja kwa mwaka mmoja ili mwanawe asafiri, aliamua kujiondoa kwenye mpango huo na kurejeshewa takriban Sh 997,000. Lakini hazina ilimweleza kuwa alihitaji kulipa Sh541,000 zaidi ili kurahisisha safari ya mwanawe.

Mzazi mwingine, Chebochok Kosgei, alieleza kuwa alilipa Sh1.177 milioni kumsomesha bintiye, lakini baadaye alitakiwa kulipa Sh541,000. Kwa kupoteza imani katika mpango huo, aliamua kujiondoa, lakini hajapokea pesa.

“Nilipoteza imani na mpango huo baada ya kutakiwa kulipa gharama za ziada kwa hivyo niliamua kujiondoa lakini sijapata kurejeshewa pesa zangu,” alisema Chebochok.

Seneta Mandago, pamoja na maafisa wa kaunti hiyo Joshua Lelei na Meshack Rono, wameshtakiwa kwa kupanga njama ya kuiba Sh1.1 bilioni zilizokusudiwa kwa mpango wa elimua ng’ambo wa Kaunti ya Uasin Gishu.

Bw Mandago pia anakabiliwa na shtaka tofauti la matumizi mabaya ya ofisi. Kesi hiyo inaendelea huku mashahidi wasiopungua 180 wakitarajiwa kutoa ushahidi wao.