Mahangaiko hoteli zikifungwa kupisha mwezi wa Ramadhani
NA FATUMA BUGU
WAKAZI wengi wa Mombasa wanaopenda mapochocho ya Pwani tayari wameanza kutafuta sehemu mbadala kukimu mahitaji yao ya kiamsha kinywa na chakula cha mchana huku Waislamu wakiendelea na mfungo.
Mikahawa mbalimbali jijini Mombasa imefungwa huku wengi wakiweka matangazo ya kufunga biashara mwezi huu wa Ramadhani na wengine wakifungua baada ya futari.
Hoteli nyingi zilizokuwa tegemeo kubwa kama Barka, Tarboush, Cafe Point na hata Kizingo zote zimefungwa mchana na kuwaacha wale wasiofunga kutaabika.
“Yani imenibidi nizunguke mjini na gari kutafuta chakula cha mchana, nimezoea Barka na Swahili Dishes lakini sasa wamefunga,” alisema Silvester Kai, mkazi wa Mombasa.
Ni dhahiri kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kunakuwa na mabadiliko mengi katika mfumo wa maisha na matendo ya watu na huwalazimu Waislamu wengi kufunga mikahawa yao wakati wa mchana. Waislamu katika kipindi hiki cha mfungo wanahitajika kujizuia kunywa na kula kutoka alfajiri (kuchomoza kwa jua) mpaka magharibi (kuzama kwa jua).
“Tumewaeleza wateja wetu katika mitandao yetu ya kijamii kuwa tutakuwa na mabadiliko na kwamba tumefunga kuanzia asubuhi hadi jioni ndipo hata wale wageni wanaokuja kutoka maeneo mengine wasitaabike,” alisema Abdhulmalik Ahmad, meneja wa hoteli ya Cafe Point.
Baadhi ya hoteli kama Barka sasa inafunguliwa kuanzia saa kumi jioni ambapo wateja wanapaswa kununua chakula na kuondoka.
“Haturuhusu mtu kula hotelini wakati huo hadi saa kumi na mbili jioni watu wanapofungua saumu ndipo wanaweza kuja, ” alisema Bw Said Nur , meneja wa hoteli ya Barka.
Hoteli ndogondogo almaarufu ‘vibandaski’ ndizo zinazofanya kazi zikiwa tegemeo kubwa kwa wanaofanya kazi jijini kwa sasa.
Biliuda Rehema, mmiliki wa mkahawa wa ‘Huda’ anasema amepoteza wateja wake waliokuwa wakinunuliwa chakula na kampuni.
“Kampuni nyingi zilizokuwa zikiagiza chakula zilikuwa za Waislamu lakini sasa hivi wamesema hadi Ramadhani iishe ndipo waanze kuagiza tena, na sasa hata wengine wakipiga simu huwa wanauliza kwanza iwapo nimefungua kwa sababu nyingi zimefungwa,” alisema Bi Rehema.
Anasema baadhi ya wateja wanaogopa kununua chakula na hata kula afisini kwani wafanyakazi wengi katika ofisi hizo ni Waislamu, hivyo inakuwa kosa au makru kula mbele yao.
“Wengi wanakuja kujificha huku ili wale kisha warudi kazini , na hao wengine tukiwapelekea tunawawekea langoni kwa kuwa hatuingii ndani ya afisi zao,” aliogeza.
Kwa sasa, hoteli nyingi zimefunguliwa saa za jioni ambapo mapochocho tele huuzwa kama vile kaimati, katlesi, bhajia, vitobosha hadi biriani na pilau. Bei za bidhaa zimekuwa kero huku wafanyabiashara wakikadiria hasara .
“Vitu havishikiki kama sasa biriani tunauza mia tano kutoka mia tatu na hamsini,” alinena Bw Nur.
Biashara nyingi za Waislamu zilizofunguliwa ni za kuuza mavazi ya kidini kama vile kanzu na manukato.
Salim Bajber, mmilili wa Qamis Thobe, duka la kuuza kanzu, anasema biashara imenoga mno kipindi hiki.
“Ramadhan ni mwezi wa neema na tunashukuru licha ya changamoto za dola wateja wako,” alisema Bw Bajber.
Manukato ya udi yamesheheni kila kona mjini huku wauzaji kama Anwar Said, mmiliki wa Red Elegence, akisema neema imetanda.
“Hivi ni vitu ambavyo hutumika sana kipindi hiki cha Ramadhan, si msikitini, si kwenye gari wala majumbani kila kitu kinaenda tunashukuru,” alisema Bw Said.