Habari za Kaunti

Majangili waua machifu 2 ndani ya saa 48

Na FLORAH KOECH, GEOFFREY ONDIEKI March 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MACHIFU wawili wameuawa kwenye mashambulizi mawili tofauti ya majangili katika muda wa saa 48 eneo la Bonde la Ufa na kuzua upya taharuki kuhusu hali ya usalama eneo hilo.

Katika tukio la kwanza, Bw Victor Sebei, naibu chifu wa Kong’asis, Tiaty Mashariki, Kaunti ya Baringo, alipigwa risasi na kuuawa Ijumaa adhuhuri katika makabiliano makali ya kufyatuliana risasi kati ya maafisa wa usalama na majangili waliojihami eneo la Chepilat.

Kulingana na Kamanda wa Polisi, Baringo, Julius Kiragu, mkasa huo ulitokea maafisa wa usalama walipokuwa wakiwaandama majambazi walioiba mbuzi na kondoo zaidi ya 70 katika uvamizi uliofanyika usiku uliotangulia katika kijiji cha Ng’aratuko, Baringo Kaskazini.

“Maafisa walikumbana na majangili Chepilat na ufyatuaji risasi ukaanza. Kwa bahati mbaya katika harakati hizo naibu chifu alipigwa risasi na kuuawa,” alisema Bw Kiragu.

Alisema haijabainika ni vipi msimamizi huyo aliishia kuwepo mahali hapo kwa sababu hakuwa sehemu ya oparesheni hiyo.Shambulizi hilo limejiri baada ya misururu ya uvamizi eneo hilo.

Wiki moja tu iliyopita, majangili walimpiga risasi na kumuua mwanamme katika eneo lilo hilo la Ng’aratuko, siku kadhaa baada ya kutoroshwa na kikosi kinachojumuisha polisi wa kawaida, polisi wa kukabiliana na dharura, polisi wa kukabiliana na wizi wa mifugo na polisi wa akiba.

Eneo hilo limeandikisha vifo visivyopungua 10 kutokana na mashambulizi ya majangili tangu mwaka ulipoanza huku wizi wa mifugo, mauaji ya kulipiza kisasi na mapigano ya jamii yakichochea uhasama.

Katika kisa cha pili, Bw Parara Lekiyierie, aliyekuwa chifu wa eneo la Pura Samburu, alipigwa risasi Jumamosi na washambulizi waliojihami waliovamia boma lake kwenye shambulizi hilo lililotekelezwa mchana peupe.

Naibu Kamishna wa Samburu, Titus Omanyi, alithibitisha mauaji hayo akiyataja “tukio la kijangili” na kumwomboleza marehemu chifu kama shujaa wa amani katika jamii.

“Alikuwa chifu aliyeheshimiwa ambaye kila mara alituliza migogoro na kuhubiri amani. Tunasikitika kumpoteza kwa namna hiyo,” alisema Bw Omanyi.

Vikosi vya usalama ikiwemo polisi na NPR vimeanzisha msako kwa wavamizi wanaoaminika kutorokea mapango karibu na eneo hilo.Mauaji hayo yameongeza idadi ya visa vya mashambulizi Samburu.

Wiki moja tu iliyopiota, watu sita waliuawa na wanane kujeruhiwa katika wizi wa mifugo eneo la Kilepoi, Baragoi.Abiria wawili walipigwa risasi na kuuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa wajambazi waliojihami kwa bunduki waliposhambulia basi lililosindikizwa na polisi kwenye barabara ya Maralal-Baragoi.