Majonzi kijana akitumbukia na kuangamia kisimani
NA MWANGI MUIRURI
WINGU la simanzi limetanda katika kijiji cha Geitwa kilichoko eneobunge la Kiharu, Murang’a, baada ya mvulana wa umri wa miaka 12 kufa maji alipoanguka katika kisima cha kina cha futi 50.
Kwa kuwa uchungu wa mwana aujuaye ni mama mzazi, mamake kijana huyo kuona mtoto ameanguka kwa kisima hicho, aliruka ndani ili kujaribu kumnusuru lakini akabahatika kunusuriwa na majirani kabla hata yeye kuzama.
Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya utawala wa mashinani eneo hilo (NGAO), mtoto huyo alikuwa akichota maji akiivuruta kwa ndoo akitumia kamba.
“Huenda alikumbwa na kizunguzungu na akaanguka ndani ya kisima hicho mnamo asubuhi ya Januari 3, 2024,” ripoti hiyo yasema.
Mamake mtoto huyo kuona hivyo, alimfuata ndani ya maji lakini kwa kuwa alikuwa amepiga nduru kabla ya kujirusha, majirani wakafika.
“Majirani waliofika walifanikiwa kumnusuru mama lakini mtoto akawa ameaga dunia,” ripoti hiyo yasema.
Iliongeza kwamba maafisa wa usalama walifika hapo na kutoa mwili na kuupeleka kwa mochari ya Murang’a.
Naye mamake alipelekwa hadi katika hospitali ya Murang’a Level 5 ambapo anatibiwa majeraha na mshtuko.