Habari za Kaunti

Uchungu wa familia ya kijana aliyepigwa na umati Timboroa kwa kushukiwa kuwa mwizi

Na MERCY KOSKEI May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIJANA mmoja mwenye umri wa miaka 28 katika Kaunti ya Baringo aliyehusishwa na wizi, alipigwa na kufa kwa uchungu katika kisa cha kusikitisha Jumatano iliyopita.

Evans Njoroge alivamiwa na kundi la watu kwa tuhuma za wizi

Nduguye mwathiriwa, Joseph Kuria anaeleza kuwa alipokea simu Jumatano iliyopita akijulishwa kuwa Njoroge alishambuliwa.

Njoroge, mchuuzi wa vyuma aliripotiwa kuzuiliwa na wakazi wenye hasira katika kituo cha Timboroa akidaiwa kuiba na rafiki yake.

Bw Kuria anasema kuwa alipofika katika eneo la tukio, alipata kakake akiwa amefungwa kwenye nguzo na kumshambulia kwa silaha  zikiwemo chuma, fimbo na nyaya za umeme.

“Maombi yake ya kutaka aachiliwe yalipuuzwa. Baada ya kupigwa, walifunga mwili wake akiwa hana fahamu kwenye pikipiki na kumvuruta kwa zaidi ya mita 100 kwenye barabara ya vumbi,” Kuria aliambia Taifa Leo.

“Nilimkuta amelala pale, akiwa amepasuka pasuka. Macho yake yalikuwa yamevimba, mwili wake ulikuwa umepigwa na singeweza kumtambua kaka yangu. Hawakumpa hata nafasi ya kuthibitisha kwamba hakuwa na hatia. Kwa nini hawangemkabidhi tu kwa polisi?” akahoji Bw Kuria.

Alipojaribu kutafuta pikipiki ya kumpeleka kakake hospitali waendeshaji pikipiki  wote walikataa wakisema walikuwa wametishwa na akambeba hadi katika Kituo cha Afya cha Timboroa.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi, madaktari walimpeleka Njoroge katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Ravine kutokana na majeraha yake.

“Ndugu yangu alifariki alipofika katika kituo hicho. Inaniuma sana kwamba walimuua. Hata kama aliiba kitu, walipaswa kumkabidhi kwa polisi,” akasema Bw Kuria.