Habari za Kaunti

Makahaba wa Thika wajitolea kulipa ushuru

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI 

VIBIRITINGOMA wanaofanyia shughuli zao katika mji wa Thika sasa wanaitaka serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto iwaweke kwa Mswada wa Fedha wa 2024 na iwatwike mzigo wa ushuru wa kati ya Sh200 na Sh400 kwa siku.

Hii ina maana kwamba sasa wanataka wawe wakitozwa Sh73,000 kwa mwaka na kwa wenye wataamua kuwa wakifanya kazi usiku na mchana wawe wakitozwa Sh400 kwa siku, hii ikiwa ni sawa na Sh146,000 kwa mwaka.

Mshirikishi wa vibiritingoma mjini Thika Bi Anne Wambui, alisema kwamba ada hizo wanazopendekeza ni sawa na zile ambazo baadhi ya polisi huwatoanisha kwa kila siku.

“Licha ya sisi kuwaona kando polisi, wao huishia kutusaliti kwa kukiuka mkataba wa maelewano. Polisi hao hutukamata na kutuwasilisha mahakamani kwa kosa hili na lile,” alisema Bi Wambui.

Bi Wambui alisema kwamba biashara hiyo yao mjini Thika, inawaleta pamoja wanawake 1,000 ambao kila siku wanaweza kuvunia serikali ushuru wa kati ya Sh73 milioni na Sh146 milioni.

Alisema kwamba badala ya vita vya kila siku kati ya serikali na wanawake hao wanaojiuza, “inafaa tuelewane jinsi tutashirikiana ndio sisi tujipe riziki nayo serikali iache kutumia vibaya rasilimali za nchi kwa baadhi ya polisi kukimbizana nasi mitaani wakiitisha hongo”.

Katika siku za hivi karibuni, wanawake hao wa kuchuuza mahaba mjini humo wamekuwa wepesi wa kutoa mapendekezo ambapo tayari wamemtaka Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi awatengee nafasi ya kungojea wateja.

“Wawekezaji wamejenga majumba na kutupea vyumba vya kuwapeleka wateja baada ya kuwatega huko mtaani. Sasa tunataka kwa kuwategea wateja kuhalalishwe na tutengewe nafasi sawa na magari ya uchukuzi ambayo huwa na steji zilizotolewa na serikali za kaunti,” akasema Bi Wambui.

Lakini Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kiambu Bw Michael Muchiri alisema kwamba pendekezo hilo halina mashiko.

“Watatusamehe kwa kuwa hadi sasa, sheria zetu zimeharamisha ukahaba na kwa ushirikiano na serikali ya kaunti, tutazidi kutekeleza misako dhidi ya makahaba,” akasema Bw Muchiri.

Aliongeza kwamba inasikitisha kuona vibiritingoma wakichafulia polisi jina kwa kuwahusisha na njama za hongo na magenge.

Alisema ripoti alizo nazo ni kwamba maafisa wa polisi wa Thika Magharibi wanafanya kazi yao vilivyo licha ya kutukanwa, kukejeliwa na kuharibiwa majina na wanawake hao.

“Katika muda wa wiki moja sasa, polisi wametia mbaroni zaidi ya wanawake 50 wa kujiuza kimwili na kufikisha kesi mahakamani. Wengi walitozwa faini ya Sh300 kila mmoja na wale walioonekana wakiwa nyanya wazee waliachiliwa huru bila masharti magumu kwa kusikitikiwa hali zao,” akasema.