• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Malandilodi Lamu warembesha nyumba bila kuvuruga upekee wa mji

Malandilodi Lamu warembesha nyumba bila kuvuruga upekee wa mji

NA KALUME KAZUNGU

WAMILIKI wa nyumba za kupangisha, almaarufu ‘malandilodi’ katika mji wa kale wa Lamu, wana kibarua kigumu cha kurembesha majengo yao bila kuvuruga upekee wa mji huo wa kihistoria.

Malandilodi hao miaka ya hivi karibuni wamelazimika kuhakikisha nyumba zao zina mwonekano bora kama njia mojawapo ya kuwavutia wateja wapangaji.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2001 mji wa kale wa Lamu uliorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuwa miongoni mwa maeneo machache yanayoenzi na kuhifadhi tamaduni na ukale wake, yaani Unesco World Heritage Site.

Ni kutokana na hilo ambapo kwa wale wanaoendeleza ujenzi mjini Lamu lazima waenende kulingana na sheria zinazofungamana na sheria za Unesco World Heritage site.

Hii ni kumaanisha hata ramani za nyumba watu wanazopaswa kujenga mjini humo lazima zikubaliwe na kupasishwa na Baraza la Mji huo.

Nyumba nyingi kisiwani Lamu hujengwa kwa ramani yenye asili ya nchini Oman, ambapo majengo hayo mara nyingi huonekana kufanana na misikiti.

Nyumba nyingi za mji wa kale wa Lamu pia zimedumu kwa miaka mingi, hivyo kuonekana kuwa sawa na magofu.

Haya yote yanatokana na ugumu uliopo kwa wamiliki wa nyumba hizo kila wanapojaribu kuzikarabati na kuhakikisha pia wanazingatia kutoharibu uhalisia au upekee wa nyumba za mji huo wa kale.

Licha ya yote, malandilodi hawajakufa moyo kwani kuna wale wanaozirembesha nyumba zao kupitia kuziweka nakshi maalum, hivyo kuwanasa kabisa wapangaji kukodisha nyumba zao.

Miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na malandilodi kuboresha mwonekano wa majengo yao bila kuharibu ukale wa Lamu ni ile ya kutumia mawe wanayoyachonga vyema na kisha kuyabandika kwenye kuta za nyumba zao kwa mpangilio au umbo Fulani.

Bw Abdulrehman Ali, mmoja wa wamiliki wa nyumba mjini Lamu anasema ingawa mtindo au ufundi wa kurembesha nyumba zao ni ghali ila wanalazimika kufanya hivyo ili wasipoteze wateja wao na pia kuwavutia wengine kukodi nyumba zao.

“Haya mawe yanayochongwa na kujengwa kwenye kuta na simiti ni ghali. Mafundi wenyewe waliobobea wakikubali kufanya kazi yako huitisha fedha nyingi. Licha ya yote hatuna budi. Usipofanya mwenzako atafanya na kuishia kuwachukua wapangaji wako wote wanaovutiwa na mwonekano mwema wa jengo au nyumba yake,” akasema Bw Ali.

Taifa Leo pia iligundua kuwepo kwa baadhi ya malandilodi walioibuka na mbinu ya kupanda au kukuza miti juu ya kuta za nyumba zao, hivyo kuleta taswira ya ukale na maandhari ya kumvutia mpangaji.

Bw Swaleh Bunu, mmoja wa wamiliki wa nyumba za kupangisha kisiwani Lamu, anasema ni kupitia mtindo wa kutia nakshi nyumba ambapo nyingi zimejaa wateja.

“Nyumba yangu iko katikati ya mji wa kale wa Lamu na vyumba vyote vimejaa wapangaji. Nimeirembesha vilivyo kupitia mtindo wa zamani na unaokubalika mjini. Wateja wakiiona huvutiwa na urembo huo. Kila wakati huulizwa kama kuna nafasi za kupangisha. Siri ni kurembesha nyumba,” akasema Bw Bunu.

Baadhi ya wapangaji waliohojiwa na Taifa Jumapili pia walikiri kuwa na ubaguzi au kuchagua ni nyumba gani wataishi na mwonekano wake uko vipi.

Picha ya nyumba na magofu yaliyorembeshwa na kuvutia kisiwani Lamu. Malandilodi wengi wana kibarua cha kurembesha nyumba zao bila kuvuruga upekee wa mji wa kihistoria wa Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Salma Athman anasema yeye hawezi kuishi kwa nyumba ambayo mwonekano wake ni wa vivi hivi.

“Hata ikiwa nyumba ni gofu lakini ikiwa imepambwa vizuri hiyo hunivutia kuishi. Ninalolikataa ni kukodi mahali ambapo maandhari ya nje ya nyumba hayavutii,” akasema Bi Athman.

Bi Sauda Mohamed anasema yeye hupendelea nyumba zilizojengwa na kuta zake kukamilishwa na simiti nyeupe ambayo mara nyingi huwa imekoleza weupe wake.

“Nawashukuru malandilodi wa siku hizi kwa kutambua hisia zetu. Naona wameibukia sana hili suala la kurembesha nyumba kwa kuzijenga na simiti nyeupe, ambapo pia uhalisia wa mji wa kale bado haubadiliki,” akasema Bi Mohamed.

Picha ya nyumba na magofu yaliyorembeshwa na kuvutia kisiwani Lamu. Malandilodi wengi wana kibarua cha kurembesha nyumba zao bila kuvuruga upekee wa mji wa kihistoria wa Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Jinsi maisha ya Mbarire yalivyogeuka baada ya kufichua...

Sakaja motoni kwa ‘kusahau’ wakazi jijini

T L