Habari za Kaunti

Malandilodi wa nyumba chafu waambiwa wapangaji si nguruwe 

May 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

KAMISHNA wa Kaunti ya Murang’a Bw Joshua Nkanatha ametoa amri kwa malandilodi wenye nyumba chafu wazingatie usafi akiwajulisha kwamba wapangaji si nguruwe.

Maafisa wa utawala walipotekeleza misako katika wadi ya Township, walibaini katika baadhi ya nyumba, mabomba ya majitaka yanavuja.

Waliwaagiza malandilodi kuwaita mafundi wa kuyakarabati huku machifu wakiamuriwa kuwa manyapara wa kuona kazi hiyo ikifanyika.

Kamishna Nkanatha aliongeza kwamba ni sharti la kikatiba kwamba serikali kuu ishirikishe kuafikiwa kwa mazingira safi, makazi yaliyo na heshima na uteja usio wa dhuluma.

Bw Nkanatha aliyekuwa akihutubia maafisa wake wa nyanjani mjini Murang’a mnamo Alhamisi alisema wamekuwa wakipokea malalamishi chungu nzima kuhusu mazingira duni ndani ya uteja wa upangaji nyumba.

“Miongoni mwa malalamishi ambayo tumekuwa tukipokea ni yale yanayohusu mabomba ya majitaka yanayovujisha uvundo na kumwaga uchafu wa vyoo katika nyumba za wapangaji,” akasema Bw Nkanatha.

Bw Nkanatha aliongeza kwamba licha ya kuwa jukumu la kutekeleza sheria za usafi ni la serikali za kaunti, serikali kuu nayo ina wajibu wa kufuatilia hali tete zinazoweza zikazua mkurupuko wa maradhi yanayoweza yakatatiza usalama na uthabiti wa nchi.

Bw Nkanatha alisema kuna baadhi ya baa ambazo hazina vyoo na ambapo walevi huenda haja ndogo na kubwa katika vichochoro vya miji.

“Aidha, kuna lojing’i ambazo hutumia vichochoro kama maeneo ya kutupa mipira ya kondomu na taulo za hedhi bila kujali hayo ni maeneo ya umma,” akasema.

Bw Nkanatha alisema kwamba Kenya ni taifa moja lililo na serikali moja na ambayo hufanya kazi kwa kusaidiana na zile za kaunti.

“Huwa tuko na wajibu wa kushirikisha huduma kwa umma kupitia kusaidiana na vitengo vingine. Wakenya wote ni wateja wa huduma za serikali na penye tunaweza tukapiga mahangaiko ya raia vita, tusiweke mipaka,” akasema.

Waziri wa Mazingira na Maji katika Kaunti ya Murang’a Bi Mary Magochi alisema kwamba malalamishi kadha yamekuwa yakiwasilishwa kuhusu hali duni za usafi katika nyumba za upangaji.

“Tunashirikiana pia na wasimamizi wa miji na mitaa pamoja na serikali kuu kuhakikisha tumekinga watu wa Murang’a kutokana na mazingira hatari na machafu,” akasema.