Mamba wafuata wakazi majumbani baada ya maji kuongezeka Ziwa Turkana
WAKAZI wa vijiji vinavyozunguka Ziwa Turkana wanapitia wakati mgumu wakikabiliana ana kwa ana na mamba wanaovamia makazi yao kufuatia kuongezeka kwa maji ya ziwa hilo.
Maji ya Ziwa Turkana yameendelea kujaa kwa kasi tangu mwaka wa 2020, hali ambayo imesababisha wakazi wengi kuhama kutoka kwa ardhi yao ya asili hadi maeneo ya juu yasiyo na huduma za msingi kama maji, afya na elimu.
Lakini zaidi ya hayo, wanalazimika kuishi kwa hofu ya kushambuliwa na mamba waliohamishwa kutoka maeneo yao ya asili.
Katika vijiji vya Apokorit, Namukuse, Lowareng’ak, na maeneo ya Lokirenoko, visa vya mamba kuwashambulia watu vimeongezeka kwa kasi.
Taarifa kutoka kwa viongozi wa eneo hilo zinaonyesha kuwa watu zaidi ya kumi wameuawa au kujeruhiwa vibaya na mamba katika kipindi cha miezi michache tu iliyopita.
“Watu wanalazimika kwenda karibu na ziwa kutafuta maji au samaki, lakini maeneo haya sasa yamejaa mamba. Wengine wanashambuliwa wakinywesha mifugo,” alisema Bw James Ekutan, mkazi wa kijiji cha Namukuse.
Wavuvi wameathirika zaidi. Wengi wanalazimika kuvua katika maeneo hatari zaidi kwani maeneo yao ya awali yamejaa maji au yamevamiwa na mamba.
Hali hiyo imewaacha kwenye hatari ya kuuawa au kujeruhiwa, huku wengine wakipoteza nyavu na mitumbwi yao kutokana na mashambulizi ya mamba.
“Hakuna msaada kutoka kwa serikali. Tumepoteza ndugu zetu na hatujapata hata pole. Shirika la Wanyamapori halijaonyesha kujali,” aliongeza Bw Ekusi, mkazi wa Apokorit.
Idara ya Huduma za Wanyamapori (KWS) imekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kusema kuwa maafisa wametumwa eneo hilo na kampeni za uhamasishaji zimeanza.
“Ni msimu wa mamba kuzaana, na wanakuwa wakali zaidi. Tunaendelea kufuatilia hali na kuchukua hatua,” alisema afisa wa KWS, Bw Elijah Chege.
Hata hivyo, viongozi wa jamii wanatoa wito kwa serikali kuanzisha maeneo salama ya uvuvi, kulipa fidia kwa waathiriwa wa mashambulizi ya wanyamapori, na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia waliohama makazi yao.
Pia wanahimiza operesheni ya kitaifa ya kudhibiti idadi ya mamba katika maeneo hatari na kuweka walinzi wa wanyama pori karibu na maeneo ya makazi.
Aidha, wakazi wanaomba mashirika ya misaada kusaidia kwa kutoa chakula, vifaa vya afya, na msaada wa kisaikolojia kwa familia zilizoathirika.
Huku mamba wakiendelea kutawala maeneo ya ziwa, wakazi wa Turkana wanalazimika kuchagua kati ya hatari ya kushambuliwa au njaa vita vya maisha ambavyo vinaendelea bila suluhisho la kudumu.