Masaibu ya Nyaribo yaendelea akisukumwa aseme Matiang’i tosha
Mwaka huu wa 2026 changamoto za kisiasa zinazomkabili Gavana wa Nyamira, Amos Nyaribo, hazionyeshi dalili za kupungua.
Kwa takribani miaka mitatu sasa, mkuu huyo wa kaunti amekuwa akijipata katika mapambano ya kisiasa yasiyokoma, huku mustakabali wake ukining’inia pabaya. Bw Nyaribo, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha United Progressive Alliance (UPA), anaonekana kuwa njia panda kisiasa.
Katika upande mmoja, baadhi ya wafuasi wake wanamsukuma kusalia imara katika mrengo wa Naibu Kiongozi wa Jubilee anayetarajiwa kuwania urais, Dkt Fred Matiang’i. Upande mwingine, kuna shinikizo ajiunge na serikali jumuishi ya Rais William Ruto kufuatia maridhiano yake na aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga.
Sintofahamu hii imezidi kuchochewa na makubaliano ya hivi karibuni ya Bw Nyaribo ya kushirikiana na Gavana wa Kisii, Simba Arati, ambaye ni mtetezi wa serikali jumuishi. Ingawa ushirikiano huo ulitajwa kama juhudi za kuimarisha umoja wa jamii ya Abagusii, umeibua mgawanyiko zaidi katika eneo pana la Gusii.
Hali ya kisiasa inayomzunguka Bw Nyaribo imekuwa tete zaidi. Hili lilidhihirika wazi alipokumbana na kelele na kejeli hadharani akiwa pamoja na Gavana Arati katika mazishi yaliyofanyika Nyamira, tukio lililoashiria kutoridhika kunakochemka miongoni mwa wananchi.
Mapokezi hayo yalikuwa ya kushangaza hasa kwa Bw Arati, ambaye kwa kawaida hupokelewa kwa shangwe kubwa katika eneo hilo.
Upinzani huo unajiri huku kukiwa na vitisho vya mara kwa mara vya kutimuliwa madarakani na hata kukamatwa, hali ambayo imekuwa ikimwandama gavana huyo na kuyumbisha azma yake ya kisiasa.
Wiki chache zilizopita, Bw Nyaribo alimtembelea Bw Arati nyumbani kwake Motonto, muda mfupi baada ya kunusurika juhudi za kumng’oa kupitia Seneti. Katika mkutano huo, viongozi hao walitangaza muungano mpya waliodai unalenga kuimarisha umoja wa Gusii na kuongeza nguvu ya eneo hilo katika siasa za kitaifa. Hata hivyo, kwa wakazi na viongozi wengi, hatua hiyo imeibua maswali mengi kuliko majibu.
Hatua hiyo ilionekana ya kushangaza hasa ikizingatiwa kuwa Naibu Kiongozi wa Jubilee, Dkt Matiang’i, ambaye pia ni mgombea urais mtarajiwa, anatoka katika eneo hilo, na magavana hao wawili hapo awali walikuwa wameashiria kuwa wangewaongoza Abagusii kumuunga mkono.
Sasa swali ni iwapo Bw Nyaribo ataweza kutuliza jahazi lake la kisiasa huku akileta manufaa ya kweli Nyamira, au kama miungano inayobadilika itaendelea kuwatenga wafuasi wake.
Aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Magharibi, Vincent Kemosi, pamoja na mwenzake wa Borabu, Ben Momanyi, ni miongoni mwa viongozi wanaoonya dhidi ya kuhusisha maendeleo na uaminifu wa kisiasa. Wamesisitiza kuwa Abagusii wanastahili huduma za serikali bila kujali wanampigia nani kura.