Mateso wauguzi wakigoma gavana akitisha kuwatimua wote
MGOMO wa wauguzi katika Kaunti ya Machakos umeingia katika kiwango cha janga la kiafya, huku wauguzi waliokuwa wamegoma sasa wakionyesha kuwa wako tayari kurejea kazini baada ya Gavana Wavinya Ndeti kutangaza mipango ya kuajiri wauguzi 500 wapya.
Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa wagonjwa katika hospitali kadhaa za umma kaunti hiyo wameachwa bila huduma, na wengi kulazimika kutafuta matibabu katika kaunti jirani za Kajiado, Kiambu, Kitui, Makueni na Nairobi.
Bi Ndeti ameagiza Idara ya Afya kuanza mchakato wa kuajiri wauguzi 500 ili kuziba pengo lililoachwa na wanaogoma, mgomo ulioitishwa na Chama cha Wauguzi Kenya (KNUN) kikidai nyongeza ya mishahara na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi.
Mgomo huo, ambao sasa umeingia siku yake ya 11, umetatiza huduma zote za afya katika hospitali za serikali ya Kaunti ya Machakos.
“Idara ya Afya imeelekezwa kuanzisha mchakato wa kuwaajiri wauguzi 500 na kuwasilisha ombi hilo kwa Bodi ya Huduma ya Umma ya Kaunti,” alisema Bi Ndeti akiwa ofisini mwake.
Aidha, ameagiza bodi hiyo kusitisha michango ya kila mwezi kwa chama cha KNUN, akitaja tuhuma za ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na mmoja wa maafisa wa chama hicho.
Nao viongozi wa KNUN tawi la Machakos walipuuzilia mbali vitisho hivyo na kumtaka gavana kushughulikia malalamishi yao badala ya kutoa vitisho.
“Chama kiko tayari kushirikiana na serikali ya kaunti kutatua hali hii inayowatesa wananchi. Vitisho vya kufukuza wanachama wetu havina msingi wa kikatiba,” alisema Michael Saka, Katibu wa tawi la KNUN, Machakos.
“Wauguzi watarejea kazini tu iwapo malalamishi yao yatashughulikiwa,” akaongeza Hesbon Mwakavi, mwenyekiti wa tawi hilo.Hii ni mara ya pili kwa wauguzi kugoma katika Kaunti ya Machakos ndani ya mwaka mmoja.
KNUN inamlaumu Bi Ndeti kwa kukosa kutimiza makubaliano ya kurudi kazini aliyotia saini mwaka jana.Mzozo huu unahusisha mkataba wa pamoja wa mwaka 2017 ulioafikiwa kati ya KNUN na aliyekuwa gavana Alfred Mutua.
“Serikali haiko tayari hata kupitia upya mkataba huo, sembuse kuutekeleza,” alisema Bw Saka.Bi Ndeti ameendelea kusisitiza kuwa matakwa ya wauguzi ni magumu mno, akitaja ukosefu wa fedha kuwa kikwazo kikuu.
“Idara ya Afya huchangia asilimia 5.78 ya mapato ya kaunti lakini hutumia asilimia 42 ya bajeti yote. Licha ya changamoto hizi, tumejitahidi kuboresha maslahi ya wahudumu wa afya,” alieleza gavana huyo.
Alisema kuwa mwaka 2023, wauguzi 132 waliidhinishwa kupandishwa vyeo kati ya wahudumu wa afya 422 waliopandishwa.
Mwaka wa 2024, wauguzi 57 waliajiriwa upya, na kufikia 2025, wauguzi 183 waliajiriwa na kupelekwa hospitalini huku 231 wakipandishwa vyeo.
“Tumeanza kuwaajiri wauguzi kwa mkataba wa muda. Nawaomba wauguzi warudi mezani kwa mazungumzo ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma,” alisisitiza.
Bi Ndeti pia alidai kuwa mgomo huo unaweza kuwa umechochewa kisiasa, ingawa hakutoa ushahidi thabiti kuunga mkono madai hayo.
Alitaja ucheleweshaji wa fedha kutoka Wizara ya Fedha kama mojawapo ya changamoto kubwa, akieleza kuwa serikali yake inalazimika kutumia mbinu mbadala za kifedha kuwalipa wafanyakazi.
Mgomo huu umesababisha hospitali nyingi kuachwa bila wahudumu huku wagonjwa wakikimbilia kaunti jirani kutafuta huduma za matibabu.
Akitoa wito wa mwisho kwa wauguzi waliogoma, Bi Ndeti alisema: “Tunaomba viongozi wa chama watambue mafanikio yaliyopatikana Machakos katika miaka miwili iliyopita. Heshima na utu wetu ni muhimu, na kuokoa maisha ndilo jukumu letu la kwanza.”