Habari za Kaunti

Matrekta yageuzwa mabasi ya shule Lamu

February 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

UBUNIFU wa Shule ya Msingi ya Mwendo Bora iliyoko katika kisiwa cha Lamu wa kugeuza trekta kuwa basi la kuwabeba wanafunzi wake, umepata umaarufu mkubwa ndani na nje ya kisiwa hicho.

Shule ya Msingi ya Mwendo Bora inapatikana kwenye kitongoji cha Sports kinachopatikana kati ya mitaa ya Kandahar na Kashmir kisiwani Lamu.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 293 ambao ni kutoka Gredi ya Kwanza hadi Gredi ya Nane.

Wanafunzi wa shule hiyo hutoka maeneo mbalimbali ambayo ni ya mbali na karibu na shule hiyo, hivyo kulazimika kubebwa na trekta-basi hilo kufikishwa shuleni kila asubuhi na kurudishwa nyumbani jioni baada ya masomo.

Taasisi hiyo ndiyo ya pekee kutumia trekta kusafirisha wanafunzi wake, hali ambayo imewavutia wengi.

Kila mara trekta lililojaa wanafunzi linapopita kwenye barabara za mji wa kale wa Lamu na mitaani, utawapata wakipinda nusra kuvunjika shingo zao kutazama ubunifu huo wa usafiri.

Kuna baadhi ambao wamekuwa wakikejeli mfumo, lakini wengi wanausifu kutokana na upekee na umaridadi wake.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Mwalimu wa Shule ya Mwendo Bora Denis Ogesa alieleza kuwa kilichowasukuma kupendelea trekta kuliko mabasi ya kawaida kubeba wanafunzi, ni changamoto za usafiri zipatikanazo kisiwani.

Shule hiyo hupatikana eneo ambalo lina mchanga mwingi, hivyo huwa ni tatizo kubwa kwa magari ya kawaida kupita bila tatizo.

Isitoshe, njia nyingi ambazo ni za vichochoro kisiwani Lamu haziruhusu mabasi makubwa makubwa kuhudumu, hivyo kuishia kutumia trekta.

“Shule ya Mwendo Bora ndiyo ya pekee inayotumia tingatinga kama njia ya kusafirisha wanafunzi wetu kwenda na kurudi kutoka shule kila siku. Pia ni ubunifu tu. Twafahamu si kawaida kuona shule ikitumia trekta au tingatinga kama namna ya usafiri wa wanafunzi wake. Tuliafikiana kutumia trekta ili kujitofautisha na shule nyingine zinazotumia mfumo wa kawaida wa usafiri ambao ni wa mabasi,” akasema Bw Ogesa.

Alishikilia kuwa walinuia kuwa shule ya kipekee inayotumia trekta kubeba wanafunzi.

Mmoja wa wazazi kisiwani Lamu, Bw Haji Shibu, alisifu ubunifu wa shule hiyo wa kuibuka na trekta-basi kwa shughuli ya usafiri.

Bw Shibu alitaja hatua hiyo kusaidia kuhifadhi hadhi ya mji wa kale wa Lamu kama eneo la Utamaduni-yaani Unesco World Heritage site.

Bw Shibu anakiri kuwa kila anapoona trekta hilo, majibu ya uamuzi huo humjia akilini.

“Ila pia nakumbuka kuwa vyombo vya kisasa vya uchukuzi haviruhusiwi hapa kwenye mji wa kihistoria isipokuwa matrekta ya kubeba taka na nyinginezo. Nimependa ubunifu wao. Trekta pia husaidia kutembea hata kwenye mchanga mwingi, hasa eneo ambako shule hiyo inapatikana. Magari au mabasi ya kawaida hayawezi kusafiri kwenye mchanga mwingi,” akasema Bw Shibu.