Habari za Kaunti

Matumaini ya kuuza mifugo ng’ambo kupitia bandari ya Lamu yaanza kufifia

Na KALUME KAZUNGU July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MATUMAINI ya wafugaji kunufaika na mpango wa serikali wa kuuza mifugo nje ya nchi kupitia Bandari ya Lamu yameanza kufifia, wengi wakisema hawajanufaika tangu mpango huo uanze mwaka wa 2022.

Serikali ilianzisha mpango huo wa kuuza fahali, mbuzi, kondoo na ngamia kutoka Kenya hadi Oman mnamo Oktoba, 2022.

“Niliwekeza pakubwa kwenye biashara ya mifugo nikitarajia ningeuza mifugo wasiopungua 30 kimataifa kila mwaka kupitia bandari ya Lamu. Kwa sasa hali ni kinyume. Hatujafahamishwa ni nini kinaendelea bandarini hapo. Imenilazimu kuuza wanyama wangu hapa nchini,” akasema Bw Noor Hassan, mfugaji wa Koreni.

Baadhi ya wafugaji wamedai kuwa, mifugo huchukuliwa kutoka kaunti za nje ya Lamu huku wao wakiachwa bila faida. Kulingana nao, wafugaji wa Lamu ndio walifaa kupewa kipaumbele katika mpango huo wa kuuza mifugo nchi za nje.

“Utapata malori yaliyojaa ng’ombe na ngamia yakitoka Garissa, Tana River, Wajir, Mandera, Turkana na kwingineko yakileta wanyama hao bandarini Lamu. Yaani kuna usiri mwingi kuhusiana na hili suala la biashara ya mifugo kupitia bandari ya Lamu kwenda nje ya nchi,” akasema Mwenyekiti wa Jamii ya Wafugaji Lamu, Bw Muhumed Kalmei.

Hata hivyo, Mamlaka ya Kusimamia Bandari Nchini (KPA) imekana madai ya ubaguzi katika mpango huo wa kibiashara.

Kulingana na KPA, mpango mzima kufikia sasa haujafikia malengo yake kwa vile huwa hakupatikani idadi ya kutosha ya mifugo kusafirishwa kwa meli hadi nchi za kigeni.

Licha ya biashara hiyo awali kupewa nafasi kubwa ya matangazo punde ilipozinduliwa, kufikia sasa ni mifugo karibu 150,000 pekee iliyosafirishwa nje ya nchi, hasa Oman, ambacho ni kiwango cha chini kuliko ilivyolengwa na kutarajiwa.

Meneja Mkuu wa Bandari ya Lamu, Bw Vincent Sidai alishikilia kuwa ni changamoto kupatikana kwa idadi inayotakikana ya mifugo ifikishwayo bandarini Lamu kusafirishwa kimataifa.

Anasema serikali imejitahidi kuboresha miundomsingi ya kusaidia biashara hiyo kunawiri ila wanaofikisha mifugo wao bandarini bado ni wachache.

“Biashara ya mifugo nje ya nchi ni miongoni mwa shughuli zinazothaminiwa sana bandarini Lamu. Changamoto ni kuwa idadi ya mifugo inayoletwa hapa bado ni ya chini. Meli moja inafaa kubeba angalau mifugo 5000 kwa awamu moja,” akasema Bw Sidai.

Alisema serikali inajitahidi kujenga gati maalumu itakayotumiwa kuingiza mifugo kwenye meli.

Ili kuboresha shughuli, kampuni ya kushughulikia biashara ya mifugo pia ilianzisha harakati zake bandarini Lamu, ambapo imekuwa ikinunua mifugo na kuimarisha afya yao kabla ya kuwasafirisha nje ya nchi.

“Ikiwa kuna wenye mifugo wanaotaka kuuza kwa wingi, waje, tutawaelekeza na hata kuwaunganisha na maajenti na kampuni za uchukuzi wa meli ili wasafirishe mifugo wao nje ya nchi. Hata mfugaji binafsi mwenye mifugo wafikao 5,000 na zaidi pia ajitokeze na tutamsaidia apate soko la tayari bandarini Lamu,” akasema Bw Sidai.