• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Mauaji ya NPR Lamu yafufua makovu kwa wakazi  

Mauaji ya NPR Lamu yafufua makovu kwa wakazi  

NA KALUME KAZUNGU

MAUAJI ya hivi punde ya askari wawili wa akiba (NPR) katika kijiji cha Ziwa La Taa, tarafa ya Witu, Kaunti ya Lamu yamezua kumbukumbu ya mashambulizi ya awali eneo hilo.

Aidha, kwa muda limekuwa likishuhudia utulivu na amani kusheheni.

NPR hao wawili waliuawa Jumamosi, Machi 23, 2024 usiku, na mwenzao akijeruhiwa vibaya mguuni pale magaidi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab walipovamia kijiji hicho.

Nyumba na pikipiki kadhaa pia ziliteketezwa na wahuni hao ambao pia waliiba vyakula na vifaa vingine vya nyumbani kabla ya kutokomea msitu wa Boni.

Ziwa La Taa ni miongoni mwa zaidi ya vijiji 20 vya Lamu ambavyo vimeshuhudia mauaji na uharibifu wa mali kufuatia mashambulizi ya Al-Shabaab.

Genge hilo lina makao yake makuu nchini Somalia.

Vijiji vingine vyenye historia mbaya ni pamoja na Juhudi, Salama, Widho, Marafa, Mashogoni, Kaisari, Ukumbi na Nyatha.

Orodha hiyo pia inajumuisha Poromoko, Mavuno Nyongoro, Mambo Sasa, Milihoi na  Lango la Simba na vingine vikiwa; Kwa Omollo, Milimani, Baure, Basuba, Bodhei, Mararani, Mangai, na Sankuri.

Utulivu ulikiwa umeshuhudiwa kiasi kwamba imani ya wakazi kuendelea kuishi maeneo hayo ilikuwa imejengeka kikamilifu.

Kwa mfano, katika mashambulio ya Al-Shabaab yaliyoshuhudiwa Lamu kati ya Juni na Septemba, 2023 na ambayo yaliangamiza zaidi ya watu 30 na nyumba zaidi ya 40, pamoja na kanisa kuteketezwa, Ziwa la Taa haikushuhudia uvamizi wowote.

Juhudi, Salama, Widho, Marafa na Mavuno, ndivyo vijiji ambavyo viliathirika na mashambulizi ya 2023.

Katika Kijiji cha Ziwa la Taa aidha, shambulio la mwisho la Al-Shabaab kuwahi kushuhudiwa lilikuwa lile la mkesha wa Krismasi mnamo Desemba 25, 2022, ambapo watu wawili waliuawa, huku nyumba tatu, pikipiki na bidhaa zingine zikichomwa.

Bi Loice Kathengi, mkazi, alisema utulivu uliosheheni eneo hilo ulijenga imani nafsini mwao kwamba mashambulio ya Al-Shabaab yalikuwa yamezikwa kwenye kaburi la sahau.

“Twashukuru kwamba serikali imejizatiti kudhibiti usalama eneo hili. Doria za walinda usalama zimeongezwa vilivyo. Isitoshe, kambi za polisi na jeshi pia zimebuniwa eneo hili. Usalama ni wa kuridhisha,” akasema Bi Kathengi.

Si Bi Kathengi pekee ambaye alikuwa amejenga imani kuhusiana na kuimarishwa kwa usalama Lamu.

Bw Safari Karisa, pia alinukuliwa akiisifu serikali kuu kwa bidii zake katika jitihada zake kukabiliana na Al-Shabaab.

Kulingana na Bw Karisa, baadhi yao walikuwa wameanza kujenga nyumba za kudumu na kuendeleza miradi mikubwa mikubwa ya maendeleo wakiwa na mtazamo mkubwa kwamba utulivu utaendelea kushuhudiwa vijijini mwao.

“Usalama umeimarishwa na ndiyo sababu miaka ya sasa utapata mtu akijijengea nyumba ya kudumu ambayo ni ya matofali kinyume na miaka ya awali ambapo watu walikimbilia kujenga nyumba madongo-poromoko.

“Zamani nyumba za matope zilipewa kipaumbele, yote yakitokana na woga wa majengo yao kulengwa na kuharibiwa na Al-Shabaab,” akasema Bw Karisa.

Hata hivyo, imani ya wakazi hao kuhusu hali halisi ya usalama wa vijiji vya Lamu iliwekwa kwenye ratili siku ya Jumamosi usiku baada ya NPR wawili kuuawa na mwingine kujeruhiwa vibaya kwenye tukio la shambulio la washukiwa wanachama wa kundi la Al-Shabaab.

Kufikia Jumapili Machi24, 2024, taharuki ilizidi kutanda miongoni mwa wakazi kijiji cha Ziwa la Taa baadhi yao wakihama kwa hofu ya kuvamiwa.

Wengi wa waliozungumza na Taifa Dijitali walisema hawawezi kuendelea kulala majumbani mwao kwa kuhofia kulengwa na kuuawa na magaidi.

Kijiji cha Ziwa la Taa kinakaribiana au kupakana na msitu wa Boni.

Kwenye mahojiano, japo waliomba kubana majina yao kwa sababu za kiusalama, walisema wahuni wa kundi la Al-Shabaab waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki na visu, walivamia kijiji cha Ziwa la Taa ambapo walikabiliana na NPR kabla ya kuwashinda nguvu na kuangamiza wawili.

Magaidi hao pia walitoweka na bunduki ya NPR.

“Walikuta NPR watatu wakishika doria kijijini Ziwa La Taa. Walianza kuwafyatulia risasi. Makabiliano makali yakazuka kwa karibu dakika 20. Kwa bahati mbaya NPR wawili waliuawa papo hapo na mwenzao akajeruhiwa mguuni kwa risasi lakini akafauli kutoroka na kujificha,” akasema afisa mmoja wa usalama eneo hilo aliyeomba tusichape majina yake.

Wenyeji wanairai serikali kukabiliana vilivyo na kudhibiti usalama Lamu.

“Shambulio la Jumamosi liwe la mwisho. Serikali iwe macho na izime kero ya Al Shabaab Lamu,” akasema Bi Mary Njeri, mkazi Ziwa la Taa.

  • Tags

You can share this post!

Siasa za Nyanza, Opiyo Wandayi akipendekezwa kumrithi Raila...

Askofu asihi Rais kuingilia kati kusuluhisha mgomo wa...

T L