Habari za Kaunti

Mbinu maalum kuzima ujangili Kerio Valley 

March 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

VYOMBO vya usalama Bonde la Kerio Valley vinapanga kutekeleza ‘mashambulizi’ kwenye maficho ya wahuni ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi kwa muda mrefu.

Kulingana na Kamishina wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Khalif Abdullahi vikosi vya usalama vinapania kuharibu maficho yote ya majangili wanaopanga kufanya uvamizi.

Mbinu hiyo, anasema itaanzia kwa kukabiliana na majangili wenyewe pamoja na familia zao.

“Kwanza, tunataka kuwatambua wenyewe na familia zao tuwavamie,” afisa huyo akasema.

Akipigia upatu mbinu hiyo, Kamanda wa Polisi Pokot Magharibi, Peter Kattam anasema watatumia familia kufuata nyayo za majangili wanaohepa mkono wa sheria.

“Hivyo, kila familia lazima ifichue wahuni hao,” Kattam akasisitiza.

Licha ya oparesheni za kiusalama ambazo zimekuwa zikifanyika, kwa muda mrefu, visa vya mashambulizi kufuatia wizi wa mifugo Bonde la Kerio vinaendelea kushuhudiwa.

Zaidi ya watu 150 wameuawa, maelfu kupoteza makazi na mali kuharibiwa chini ya kipindi cha mwaka moja uliopita.

Kulingana na Bw Kattam, familia za majangili zitabeba mzigo kufidia waathiriwa wa madhila yao.

“Familia zitarejesha mifugo walioibwa, kulipa faini, kugharamia uharibifu; walioumia na kuuawa,” akaelezea.

Isitoshe, kigogo huyo wa polisi Pokot Magharibi alisema familia za wahusika zitawajibika kusalimisha silaha za polisi zilizoibwa na kutumika kutekeleza unyama.

“Ifahamike wazi kuwa watasimamia gharama ya nauli ya maafisa wa usalama na wazee wanaofuata mifugo walioibwa na wanaoibwa,” akasema.

Huku ukosefu wa elimu miongoni mwa wakazi na mizozo ya ardhi ikitajwa kama mojawapo ya sababu kuu za wizi wa mifugo na mashambulizi ya mara kwa mara, alisema serikali inatathmini kusaka suluhu kwa kuangazia gapu hizo.

Anasisitiza haja ya wenyeji kupata hatimiliki za ardhi na mashamba yao, hususan katika jamii za wafugaji.

Vilevile, mipango ya kamati za kuchunga mifugo imebuniwa kufanikisha amani katika Bonde la Kerio Valley.

Wazee na wachungaji wamefufua mbinu za kitamaduni kulinda mifugo ili kukomesha ujangili na wizi wa mifugo ambao kwa kiasi fulani hupepetwa na athari wa mabadiliko ya tabia nchi.

Kamati ya watu 20 kutoka jamii za Pokot, Turkana na Elgeyo Marakwet zimebuniwa kusaidia kutatua mizozo ya mara kwa mara.

Miongoni pia mwa mikakati inayolengwa ni kuibuka na mbinu za kulisha mifugo na kuwapa maji.

Mratibu wa shirika la Safer World, Elizabeth Atieno alisema watajumuisha viongozi wa kidini katika kuleta amani kaunti za Pokot Magharibi, Turkana na Elgeyo Marakwet.

“Tunataka viongozi wa kidini wawe mabalozi wa amani katika jamii,” akasema.

Baraza la jamii ya Pokot, aidha, limeanzisha mchakato kufanya mazungumzo na wenzao wa Turkana na Marakwet kuhusu mzozo wa mipaka, ambao pia umechangia vurugu.

“Tutatumia mbinu za kitamaduni na tutakomesha ujangili,” alisema mwenyekiti wa baraza hilo, Bw John Muok.

Chesegon, Turkwel, Kainuk na Kapedo, ni kati ya maeneo hatari Bonde la Kerio ambayo familia nyingi zimepoteza wapendwa wao.

Waziri wa Usalama, Prof Kithure Kindiki amekuwa akizuru eneo hilo hatari, na hata kufanya mageuzi ya uongozi katika asasi za usalama na utawala wa kimikoa.