Mbinu za kina mama kukabiliana na wizi wa mifugo
NA OSCAR KAKAI
HUKU serikali ikijikakamua kupambana na visa vya wizi wa mifugo na mashambulizi ya mara kwa mara Pokot Magharibi, baadhi ya mashirika yanajituma kuunganisha kina mama katika kaunti hiyo na kuwaundia jukwaa kujiendeleza kimaisha.
Mashirika hayo, yanahamsisha uzinduzi wa makundi wanayoyatumia kuendeleza kilimo na sanaa – kuunda bidhaa.
Wanawake hao wanaoendeleza shughuli hiyo kupitia makundi, wanatumia shanga kuunda bidhaa maridadi.
Ni jukwaa wanalotumia kudumisha amani eneo hilo, ikizingatiwa kuwa baadhi yao na waathiriwa wa mashambulizi ya wizi wa mifugo.
Awali, shanga zilichukuliwa tu kama sanaa kuonyesha mila na utamaduni, ila sasa wamezigeuza kuwa hela.
Monica Silinyang ni mmoja wao, anayenufaika na mpango huo kupitia Shirika la Village Enterprise na anasema washirika wamepewa mafunzo kuongeza shanga thamani ili kuteka fedha.
“Tumebuni vikundi ambapo tunaweka fedha na kukopeshana,” akaambia Taifa Leo Dijitali.
Katika kilimo, Mary Cherotich mkazi wa eneo la Morpus anasema kuwa wanapanda mboga na mimea mingine kama vile mahindi ili kukabiliana na njaa.
“Kwa sasa, tunaweza kulisha watoto wetu na kupigana na athari za mabadiliko ya hali ya anga,” anasema.
Huku wakikumbatia teknolojia na mifumo ya kisasa, kama vile mashamba ya mabustani, anasema kuwa hawahitaji kiwango kikubwa cha ardhi kuzalisha chakula.
“Ni kazi rahisi. Wakazi wengi walikuwa wanaogopa kufanya kilimo kwa sababu ya kiangazi. Mimi hutumia maji kidogo sana kunyunyizia mimea yangu,” anasimulia.
Changamoto ya kununua mboga bei ghali, kwake sasa ni historia.
Isitoshe, mazao anayovuna Cherotich anasema anauza na kupata hela kusomesha wanawe.
Aidha, wamefunzwa mseto wa mifumo kuendeleza kilimo cha kisasa.
Caroline Menach mwalimu mkuu Shule ya Mtatifu Elizabeth na mratibu katika Shirika la Perur Ray of Hope kwenye majojiano, alisema kipande kimoja cha shamba kinaweza kupandwa mimea miche 100 ya mboga.
Wanalima sukuma wiki, spinachi, kabichi na karoti.
“Kina mama wanapata chakula na hata kuingiza mapato kujiendeleza kimaisha,”alisema.
Leah Okero, Mkurugenzi Shirika la Village Enterprise Kenya anasema kuwa mpango kupiga jeki kina mama hao unalenga kubuni nafasi za kazi na kubadilisha maisha ya wanawake katika jamii za wafugaji.
Anasema wanapewa mafunzo jinsi ya kuwekeza kutumia raslimali walizonazo.
“Kila mwaka sisi husaidia maboma yapatayo 1,080 ambapo asilimia 80 ni wanawake katika Kaunti ya Pokot Magharibi. Sisi huwapa mafunzo ya kiuchumi, kibiashara na kuwapa fedha waanzishe biasharia,” anasema afisa huyo.
Cha kutia moyo, kupitia kilimo cha mseto wa mimea wameweza kuangazia visa vya utapiamlo hususan miongoni mwa watoto.
“Miradi ya aina hii eneo kama Pokot Magharibi ambapo visa vya visu vya ngariba kwa wasichana vinaendelea kushuhudiwa, tunaitumia kuhubiri athari za ukeketaji,” Okero anasema.
Hali kadhalika, wanatumia mipango ya kuwainua kimaisha kuwahamasisha kujitoza kwenye uongozi, katika ngazi ya serikali kuu na ya kaunti.
Peris Chepanga’t afisa kutoka Shirika la Deutsche Stiftung Weltbevölkerung (DSW) anaainisha jukumu la mwanamke katika kuinua jamii.
“Unapoinua mwanamke, jamii inakua,” Peris anaeleza.
Hata hivyo, anasema kuwa bado kuna changamoto ambapo mwanamke bado anadhalilishwa na kunyimwa nafasi kuinuka.
Kwa fulani fulani, visa vya ukeketaji vinaathiri Pokot Magharibi.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la International Tree Foundation (ITF) anasema kuwa wanawake chini ya kikundi cha Perur Rays of Hope wanalenga kulinda mazingira kwa kupigana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuondoa ukame, kutunza na kuongeza idadi ya miti 50,000 kufikia Aprili 2024.