Habari za Kaunti

MCA wapinga madai ya kumng’atua gavana mamalakani

Na LUCY MKANYIKA September 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAWAKILISHI wa wadi wa Kaunti ya Taita Taveta wamepinga madai kuwa kuna njama ya kumng’atua mamlakani Gavana Andrew Mwadime.

Hayo yanajiri baada ya madai kuibuka kuwa bunge la kaunti hiyo linapanga kumtoa gavana huyo kutokana na masuala mengi yanayokabili serikali yake.

Wakiongea katika eneo la Sagalla, wawakilishi hao walisema kuwa madai hayo hayana msingi wowote kwani wako tayari kufanya kazi na Gavana Mwadime bila malumbano.

Mwakilishi mteule Rose Shingira alisema kuwa bunge hilo litafanya kazi na gavana huyo kwa manufaa ya wananchi.

“Nasikia watu fulani wanaeneza uvumi kuwa tumefanya vikao usiku vya kujadili masuala ya kuleta mswada wa kumng’oa Gavana Mwadime. Hayo yote ni ya uongo,” alisema.

Alisema kuwa wanaoleta uvumi huo ni wapinzani wanaolenga kuleta uhasama kati ya bunge hilo na Gavana Mwadime.

“Nakuhakikishia gavana kuwa tuko nyuma yako. Tunakuomba uendelee kufanya kazi bila uoga wowote,” alisema.

Wakati huohuo, Gavana Mwadime alisema kuwa upinzani unataka kulemaza serikali yake kwa kusambaza propaganda ili wananchi wakose imani naye.

Alisema kuwa wanaopinga serikali yake wamezua madai ya uongo kuwa baadhi ya maafisa wake wamefuja fedha za umma.

“Wanataka waseme kuwa nimeshindwa na uongozi. Ndio maana wanabuni mambo ya kudai kuwa wawakilishi wanataka kuning’oa ilihali walikuwa kwa mkutano mwingine tofauti,” alisema.